Huenda watu milioni 6 wakafa njaa Sudan Kusini
5 Mei 2017Onyo hili linakuja wakati ambapo jamii ya kimataifa ikipambana kuchangisha dola bilioni 4.4 kuepusha janga kamili. Ukosefu huo wa chakula katika taifa hilo changa zaidi duniani, ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa katika mkutano wa jukwaa la kimataifa la kiuchumi kwa Afrika uliofanyika mjini Durban, Afrika Kusini, ukiwaleta pamoja wafanyabiashara na wanasiasa wakuu barani humo.
Saira Khan afisa mkuu mtendaji wa shirika la misaada la Stop Hunger Now Southern Africa, alionya kwamba hatua ya jamii ya kimataifa kutoishughulikia vyema hali ya Sudan Kusini, inatishia maisha ya mamilioni ya watu.
"Bado hakuna mwangaza. Tunaona hali ya kutoelewana baina ya mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali zenyewe, kuhusiana na linalohitajika kufanyika," alisema Khan. "Ni hali ngumu kwa eneo hilo na iwapo hatutofanya lolote huenda tukashuhudia watu milioni 6 wakipoteza maisha yao kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwasababu ya njaa."
Uhaba wa fedha ndicho kitisho cha maisha ya watu
Mwezi Februari, Sudan Kusini na Umoja wa Mataifa walitangaza rasmi ukame unaoathiri zaidi ya watu 100,000 katika baadhi ya sehemu ya eneo kubwa la Unity, hali ambayo Umoja wa Mataifa ulisema kwamba ni janga lililosababishwa na wanadamu na kwamba lingeweza kuepukika.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la Oxfam Winnie Byanyima, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba, uhaba mkubwa wa fedha za kusaidia katika juhudi za kutoa misaada ndilo jambo linalotishia maisha.
Umoja wa Mataifa unasema kati ya dola bilioni 4.4 zinazohitajika kufikia mwezi Julai ili kuzuia kufariki kwa idadi kubwa ya watu, ni asilimia 26 pekeyake ya fedha hizo zilizopatikana.
Zaidi ya watu milioni 1.9 ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan Kusini na takriban wengine milioni 1.7 wamekimbilia usalama wao katika nchi jirani. Jumla ya wakimbizi 830,000 kutoka nchini humo wamekimbilia Uganda na Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba idadi hiyo itafikia milioni moja kufikia katikati ya mwaka huu.
Nigeria huenda ikakabiliwa na janga la kivyake la njaa
Byanyima alitoa wito wa kuufanyia mageuzi Umoja wa Mataifa, ili kuzikabili changamoto za Sudan Kusini. "Hii leo Umoja wa Mataifa umekuwa dhaifu kabisaa kiasi ya kwamba, hauwezi hata kulifanya Baraza la Usalama kuwatia mbinyo viongozi wasiowajibika kama wale wa nchini Sudan Kusini," alisema Byanyima.
Sudan Kusini ilitumbukia kwenye machafuko Disemba mwaka 2013 kufuatia mzozo wa madaraka baina ya rais Salvar Kiir na aliekuwa makamu wake Riek Machar.
Kwengineko Afrika, Byanyima alionya kuwa huenda Nigeria ikakabiliwa na janga la kivyake la chakula. "Nimetoka kuzuru eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria, eneo lililoharibiwa na Boko Haram, kuna watu 47,000 katika eneo hilo wanaoishi katika mazingira yenye ukosefu wa chakula na wengine milioni tano huenda wakakabiliwa na hali hiyo katika miezi michache ijayo," alieleza mkurugenzi huyo wa Oxfam.
Mashirika ya kutoa misaada kaskazini mwa Nigeria yataishiwa na pesa za kuzuia upungufu wa chakula ifikiapo mapema mwezi Juni na haya ni kwa mujibu wa naibu mratibu wa misaada ya kibinadamu nchini Nigeria, Peter Lundberg.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga