Mawasiliano ya simu kati ya UAE na Israel yarejea hewani
17 Agosti 2020Baraza la ushirikiano katika mataifa ya Ghuba GCC, limelaani vitisho vilivyotolewa na rais wa Iran na maafisa wengine wa nchi hiyo, dhidi ya Umoja wa falme za kiarabu UAE, baada ya kufikia makubaliano ya kurekebisha mahusiano yake na Israel.
Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu umefanya kosa kubwa kufikia makubaliano hayo na Israel, akilaani kile alichokiita kuwa ni usaliti wa taifa la Ghuba. UAE ilijibu kwa kumuita balozi wa Iran nchini humo kufuatia matamashi ya rais Rouhani, iliyoyaelezea kuwa ni vitisho.
Huduma za simu baina ya UAE na Israel zilianza tena kufanya kazi Jumapili na kuashiria hatua muhimu ya mahusiano ya kidiplomasia yaliyoratibiwa na Marekani yaliyoitaka Israel kusimamisha mipango yake ya kutwaa ardhi inayopiganiwa na Wapalestina.
Mawasiliano ya simu za moja kwa moja yalikatwa katika taifa hilo la kifalme linaloundwa na falme ndogo saba na ambalo ni mshirika wa Marekani, tangu kuundwa kwake mwaka 1971. Maafisa wa UAE wamethibitisha kuwa waziri wake wa mambo ya kigeni Sheikh Abdullah bin Zayed al Nahyan alimpigia simu mwenzake wa Israel Gabi Ashkenazi. Baadae waziri wa habari wa Israel Yoaz Hendel alitoa taarifa akiipongeza UAE kwa kufungua mawasiliano.
"Ningependa kuwapongeza marafiki zangu kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kufungua simu za moja kwa moja kutoka taifa la Israel. Hii ni hatua iliyobarikiwa na muhimu ambayo ni mwanzo wa njia ndefu na fursa mbalimbali za kufanya kazi pamoja. Israel na UAE zina uwezo usio na mwisho wa ushirkiano wa kiuchumi, kitamaduni na kidiplomasia. Mawasiliano ya simu ni njia muhimu ya kuanza. Salaam Aleikum marafiki", alisema waziri wa habari wa Israel.
Israel na Umoja wa Falme za kiarabu zilitangaza siku ya Alhamis kuwa zinaanzisha mahusiano ya kidiplomasia katika mpango ulioratibiwa na Marekani. Makubaliano hayo yaliashiria ushindi wa kihistoria katika sera za kigeni za rais Donald Trump anayetafuta kuchaguliwa tena. Waziri mkuu Benjamin Netanyahu alisema jana kwamba makubaliano hayo yanaonyesha dhahiri kuwa Israel haihitaji kujiondoa katika ardhi iliyotwaliwa inayotafutwa na Wapalestina ili kuweza kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa ya kiarabu.
Mikataba kadhaa baina ya nchi hizo mbili inatagemewa kusainiwa wiki zijazo, hususan katika sekta za utalii, ndege za moja kwa moja na kufungua balozi. Tayari kampuni ya UAE imetia saini na kampuni ya Israel kwa ajili ya kufanya utafiti wa janga la virusi vya corona. Hata hivyo makubaliano hayo yamechochea hasira miongoni mwa wale walioona kama kitendo cha usaliti wa juhudi za muda mrefu za kuanzisha taifa huru la Palestina. Nchini Pakistan mamia waliandamana kupinga makubaliano hayo.
Vyanzo: AP/AFP/Reuters