1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Kulitendeka uhalifu wa kivita Amhara

4 Aprili 2024

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaka Umoja wa Mataifa uchunguze uhalifu wa kivita uliofanywa na jeshi la Ethiopia katika eneo la Amhara, ambalo limekuwa likizongwa na mizozo.

https://p.dw.com/p/4eQ4I
Waandamanaji wa jamii ya Amhara.
Waandamanaji wa jamii ya Amhara.Picha: Marcello Valeri/ZUMA/picture alliance

Tume ya Haki za Binadamu ya Ethiopia ilikadiria mwezi Februari kwamba watu wapatao 45 waliuliwa siku ya tarehe 29 Januari na vikosi vya serikali katika mji wa Merawi kufuatia mapigano na wapiganaji wa kundi la Fano.  

Vile vile, shirika la Human Rights Watch liliutaka Umoja wa Afrika usitishe upelekaji wa vikosi vya serikali ya Ethiopia kwenye tume za amani mpaka makamanda waliohusika na ukiukaji huo mkubwa wa haki watakapowajibishwa.

Soma zaidi: Licha ya mwaka mmoja wa mkataba wa amani, mapigano yanaendelea Ethiopia

Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika, Laetitia Badr, alisema kushindwa kwa serikali ya Ethiopia kuhakikisha vikosi vyake vinawajibishwa kwa ukiukaji huo jimboni Amhara kunachangia kurejelewa kwa machafuko kila mara na kufanya uhalifu bila kujali kuchukuliwa hatua za kisheria.