1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaitaka dunia ilaani ukandamizaji Rwanda

29 Septemba 2017

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limeitaka jumuiya ya kimataifa kulaani vitendo vya ukandamizaji vinavyofanywa na serikali ya Rwanda dhidi ya wapinzani na wakosoaji wa serikali hiyo.

https://p.dw.com/p/2kx5n
Ruanda Präsidentschaftswahlen Kampagne Präsident Paul Kagame
Picha: Reuters/J. Bizimana

Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo la haki za binaadamu na kusambazwa kwa vyombo vya habari inasema ukandamizaji huo unaofanywa na serikali ya Rwanda unamaanisha kuwa utawala huo hauko tayari kuwavumilia wakosoaji wake au kukubali dhima ya vyama vya upinzani.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika ukanda wa Afrika ya Kati, Ida Sawyer, amesema kwenye taarifa hiyo kwamba hatua hizi za serikali ya Rais Kagame zinakusudiwa kutuma ujumbe wa vitisho kwa wale wanaojaribu kuukosoa utawala.

"Katika kila mtu mmoja anayekamatwa nchini Rwanda, wanaothubutu kuzungumzia dhidi ya sera ya dola au mateso wanazidi kupungua," anasema mkurugenzi huyo.

Miongoni mwa watu wa karibuni zaidi kulengwa na ukandamizaji huo wa dola, linasema shirika hilo, ni aliyetia nia kuwania urais kwenye uchaguzi uliopita dhidi ya Rais Kagame, Bi Diane Rwigara, pamoja na familia yake na wafuasi wao, sambamba na viongozi kadhaa wa chama cha upinzani cha FDU-Ikingi.

Baada ya kukanusha mara kadhaa kuwashikilia au kujuwa ripoti zao, baadaye polisi nchini Rwanda imekiri kuwashikilia Bi Diane Rwigara, dada na mama yake, ambao kwa pamoja wameshitakiwa kwa makosa yanayohusiana na kodi na pia kutoa taarifa za siri hadharani.

Mashitaka dhidi ya wapinzani

Ruanda Diane Rwigara
Diane Rwigara, ambaye yeye na mama na dada yake, wanashikiliwa na serikali ya Rwanda kwa mashitaka ya kutoa siri na kodi.Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

Mnamo tarehe 6 Septemba, maafisa wa usalama pia waliwakamata wanachama wa ngazi za juu wa chama cha upinzani cha FDU-Inkingi, akiwamo Makamu wa Rais wa chama hicho, Boniface Twagirimana, mkuu wa uhamasishaji Fabien Twagirayezu, msaidizi mweka hazina Leonille Gasenyire na kamishna msaidizi Gratien Nsabiyaremye. 

Mwakilishi wa chama hicho mjini Kigali, Theophille Ntirutwa, hajuilikani alipo tangu tarehe 6 mwezi huu. Viongozi hao pamoja na wanachama wengine sasa wamefunguliwa mashitaka ya kuunda kundi la silaha na kumtukana rais.

Licha ya kwamba ilishakuwa dhahiri kuwa Rais Kagame angelirejea tena madarakani kwenye uchaguzi wa hapo Agosti 4, viongozi wa serikali yake waliamua kuendesha kampeni kali dhidi ya yeyote aliyejitokeza kumpinga kiongozi huyo wa muda mrefu nchini Rwanda.

Human Rights Watch inasema katika taarifa hiyo iliyotolewa baada ya kuzungumza na wanaharakati na raia wa kawaida, kuwa wagombea kadhaa wa urais walizuiwa kushiriki uchaguzi huo, na wale wawili walioruhusiwa - Frank Habineza na Philippe Mpayimana - walisema walitishiwa maisha na kubughudhiwa.

Shirika hilo la haki za binaadamu linaitaka serikali ya Rwanda kuchunguza na kutoa taarifa ya haraka ya matukio hayo ya kukamatwa watu kinyume na sheria na kuwatendea vibaya raia, likisema kwamba ni kinyume na sheria za Rwanda na za kimataifa.

Vile vile, Human Rights Watch imezitaka nchi wafadhili na jumuiya ya kimataifa kulaani ukandamizaji unaoendelea nchini Rwanda dhidi ya wapinzani wa kisiasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/HRW
Mhariri: Saumu Yussuf