1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Unyanyasaji wa wanaharakati wa amani waongezeka Myanmar

1 Februari 2019

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema serikali ya Myanmar chini ya mshindi wa tuzo ya kimataifa ya Nobel Aung San Suu Kyi ilitumia sheria kandamizi kuwashitaki wanaharakati

https://p.dw.com/p/3CYYX
Myanmar Gericht weist Berufung von Reuters-Reportern ab - Ehefrauen der Journalisten
Picha: Getty Images/AFP/Sai Aung Main

Ripoti hiyo ya Human Rights Watch imesema uhuru wa kujieleza umezidi kudhoofika tangu utawala wake ulipoingia mamlakani mnamo mwaka 2016, katika wakati ambapo mashitaka yakiibua kile ilichokiita "mazingira ya hofu" miongoni mwa waandishi wa habari.

Mshauri wa masuala ya sheria wa Asia katika shirika hilo, Linda Lakhdhir amesema kwenye taarifa yake kwamba Aung San Suu Kyi pamoja na chama chake cha National League for Democracy waliahidi Myanmar mpya, lakini serikali yake bado inatuhumu hotuba na maandamano ya amani na imeshindwa kurekebisha sheria kandamizi za zamani.

Hata hivyo msemaji wa serikali hakupatikana mara moja kujibu tuhuma hizo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya kijeshi inayotawala Myanmar kwa miongo kadhaa imeweka sheria kali dhidi ya uhuru wa kujieleza. Marekebisho yaliyofanywa na serikali ya kiraia iliyoingia mamlakani mwaka 2010 ikiwa ni pamoja na kufutiliwa mbali kwa udhibiti, kulisababisha matokeo chanya katika masuala ya uhuru wa habari na hata mikusanyiko.

Aung San Suu Kyi Regierungschefin von Myanmar
Utawala wa Aung San Suu Kyi unatuhumiwa kwa unyanyasajiPicha: picture-alliance/dpa/B. Marquez

Kundi linalopigania uhuru wa kujieleza la Athan la nchini Myanmar, ambalo ripoti yake ilitumiwa na shirika hilo la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema takriban kesi 140 zimewasilishwa mahakamani tangu mwaka 2016 chini ya sheria ya mawasiliano, na angalau nusu ya kesi hizo zilihusisha madai dhidi ya uhuru wa kujieleza.

Bunge lilifanya mabadiliko ya kifungu cha 66(d) cha sheria kinachotoa adhabu ya kifungo cha hadi miaka miwili jela kwa mtu yoyote anayeharibu sifa ya mtu mwingine kwa kutumia mitandao ya mawasiliano. Pamoja na miito, lilikataa kubatilisha kifungu hicho.

Waandishi wa habari ndio walikuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko haya pamoja na kushambuliwa, imesema ripoti hiyo, huku pia wakikabiliwa na vitisho. Matokeo ya haya yameibua mazingira ya hofu miongoni mwa waandishi wa habari wa nchini humo.

Sheria za uhalifu wa kuchafua majina ya wengine, sheria ya siri za serikali, mashirika yasiyo ya halali, sheria ya ndege pamoja na kanuni ya 131 ya Adhabu, kwa pamoja zimekuwa zikitumika dhidi ya waandishi wa habari katika miaka ya hivi karibuni nchini humo.

Waandishi wa habari wa shirika la habari la Reuters Wa Lone na Kyaw Soe Oo walihukumiwa kifungo cha miaka 7 gerezani mnamo mwezi Septemba, 2018 chini ya sheria ya enzi ya ukoloni ya Siri za Serikali. Wamekuwa wakifanya uchunguzi kuhusu mauaji ya wanaume na wavulani 10 wa jamii ya Waislamu walio wachache wa Rohingya katika jimbo la Rakhine.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE
Mhariri: Josephat Charo