1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Serikali ya Marekani itoe maji safi kwa raia wake

8 Septemba 2021

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch limelitaka bunge la Marekani kuunga mkono programu zinazohakikisha raia wa nchi hiyo wanaweza kupata maji safi na salama.

https://p.dw.com/p/4050X
Bildergalerie Detroit USA Neues Leben nach der Insolvenz
Picha: Getty Images/Joshua Lott

Wakati huo huo serikali ya Marekani itambuwe kwamba maji safi na salama ni haki ya kimsingi ya binaadamu.

Ujumbe uliotolewa na shirika hilo kwa njia ya video unalitaka baraza la Congress lichukuwe hatua za makusudi kuhakikisha upatikanaji wa haki ya maji salama na huduma za maji machafu kwa raia wote wa Marekani. Kauli hiyo inakuja wakati bunge hilo la Marekani likijadili mswaada wa sheria wa bajeti ya miundombinu, ambao unahusisha ufadhili wa programu ya maji salama kwa wote.

Amanda Klasing, mkurugenzi wa haki za wanawake na mtaalamu wa haki za maji na usafi katika shirika la Human Rights Watch, amesema ambapo watu wengi Marekani wanadhani ni jambo la kawaida kufungua mfereji na kupata maji majumbani mwao, haki hiyo ya kimsingi hawanayo mamilioni ya familia za Kimarekani hazina fursa hiyo.

Familia nyingi zimeathirika na ukosefu wa maji safi Marekani

Bibi Klasing ameongeza na hapa namnukuu: "Kutokana na miundombinu ambayo imeshazeeka, mabadiliko ya tabianchi na janga la kilimwengu la corona, Congress inapaswa kuhakikisha kwamba nyumba na familia ambazo zimeathirika vibaya zaidi zinapata huduma hii wanayoihitaji haraka sana." Mwisho wa kumnukuu.

400 000 ohne Trinkwasser in Ohio
Raia wa jimbo la Ohio akinunua majiPicha: picture-alliance/dpa


Kukosekana kwa uwekezaji na msisitizo kwenye usawa na upatikanaji wa huduma ya maji kumekuwa na athari mbaya kwa familia nyingi za Kimarekani zenye kipato cha chini, hasa wenye asili ya Kimarekani, wenyeji wa asili wa taifa hilo na jamii nyengine za wachache.

Zaidi ya hapo, kukosekana kwa taarifa za uhakika kumefanya iwe shida kwa jamii hizo kufuatilia uvunjaji huo wa haki yao kimsingi ama kuwashinikiza maafisa wa serikali kusaka suluhisho la tatizo hilo.

Hata ilipodhihirika wazi kwamba mzozo wa maji salama unakuja juu nchini Marekani, serikali kuu imekuwa haitaki kuutambuwa wajibu wake mbele ya sheria ya haki za binaadamu ya kimataifa ambayo inazitaka serikali ulimwenguni kuhakikisha maji salama na huduma za usafi kwa watu wake.

Mnamo mwaka 2019, kwenye kupitishwa azimio la haki ya maji kwa walimwengu, mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa alisema "Tunapingana na dhana yoyote kwamba haki ya maji salama imeungana moja kwa moja na haki nyengine za binaadamu, kama vile haki ya kuishi." 

Serikali kuu na za majimbo hazina wajibu wa takwimu za maji

Mashirika ya haki za binaadamu ya kimataifa yameonesha wasiwasi wao kwa miaka kadhaa kwamba Marekani inashindwa kutimiza wajibu wake wa kuhakikisha haki za maji salama na huduma za usafi zinatimizwa ipasavyo.

Kisheria, serikali kuu ya shirikisho wala za majimbo hazina wajibu wa moja kwa moja wa kuweka takwimu juu ya upatikanaji maji, licha ya kwamba haki za binaadamu zinasema kwamba kila mtu anastahiki kupata maji salama kwa matumizi yake binafsi na ya nyumbani.

USA Trinkwasser in der Stadt Flint vergiftet
Mfanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu akimsaidia mkaazi wa Michigan na majiPicha: Getty Images/S. Rice

Tatizo hili limeongezwa makali na janga la COVID-19 na shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch linasema janga hilo linalazimisha kwamba jamii ambazo miaka mingi zimetengwa na huduma hiyo muhimu zinakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuathirika na kusambaza virusi vya corona.

Tangu kuanza kwa janga la COVID-19 mwezi Machi 2020, watetezi wa haki za kiafya na za binaadamu wameongeza shinikizo lao kwa serikali ya Marekani wakiitaka kutambua haki ya maji kwa kukomesha tabia ya serikali za majimbo na makampuni ya maji kufungia huduma hiyo kwenye nyumba zilizoshindwa kulipia.

Baraza la Congress, kwenye moja ya maazimio yake ya mfuko wa kutoa nafuu ya kiuchumi kutokana na madhara ya janga la COVID-19, lilitenga zaidi ya dola bilioni moja kwa ajili ya kuanzisha Programu ya Msaada ya Maji kwa Familia za Kipato cha Chini, LIHWAP, ili kuzisaidia familia hizo kulipia gharama za maji salama na maji machafu.

Lakini programu hii ni ya kipindi kifupi tu na ya dharura, sio ya kudumu kama wanavyotaka wanaharakati, na licha ya hayo inakosolewa kwa kuweka vigezo vya kibaguzi kwa watu wanaoshiriki.