Hongkong,Uhai anuai na Uchumi wa Ujerumani Magazetini
14 Agosti 2019Tunaanzia Hongkong ambako vuguvugu la maandamano limehamia katika uwanja wa ndege na kukorofisha shughuli zote za usafiri kwa siku ya tatu mfululizo katika jimbo hilo muhimu kiuchumi. Vikosi vya usalama vinatunisha misuli. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika: "Nchi za magharibi zinabidi hivi sasa zisimame kidete kudai demokrasia iheshimiwe.Ikimaanisha uheshimiwe uhuru wa watu kuitisha mikutano, kuachiwa huru wanaharakati waliokuwa wakiandamana kwa amani na polisi iache kutumia nguvu. Hadi wakati huu nchi za Ulaya zilikuwa zikielemea zaidi upande wa China katika vita vyake vya kibiashara dhidi ya Marekani. Hawajakosea. Lakini ikiwa damu itamwagika Hongkong , Ujerumani na nchi za Ulaya hazitakuwa na budi isipokuwa kubadilisha msimamo huo."
Juhudi za kuhifadhi uhai anuai
Juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ziko na ni za aina tofauti, miongoni mwazo ni kuhifadhi uhai anuai. Gazeti la mjini Lüneburg "Landeszeitung" linachambua wapi juhudi hizo zimefikia: Gazeti linaandika: "Serikali ya Marekani inapunguza makali ya sheria ya mwaka 1973 kuhusu hifadhi ya uhai anuai. Rais Bolsonaro wa Brazil amepania kulitumia eneo la Amazon kwa masilahi ya kiuchumi. Na Ujerumani je? Baraza linaloshughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi lilikutana kwa kikao chake cha tatu, majadailiano yalikuwa makali lakini bila ya matokeo yoyote. Ukweli ni mchungu. Hakuna yeyote kati ya madola makuu aliyejifunza chochote kile. Naiwe kutokana na madhara yanasosababishwa na hali ya hewa, au ukame, mmomonyoko wa ardhi au kupungua kwa sehemu kubwa uhai anuai. Mpaka ripoti ya kutisha kuhusu hali ya mazingira namna ilivyo haikusaidia kitu. Licha ya kwamba ripoti hiyo imebainisha hakuna tena wakati si wa majadailiano wala si wa kisingizio. Suala sio tena kuhusu uwiano kati ya uchumi na mazingira. Sio tena kama hatua za kukabiliana na kuchafuliwa mazingira zinaweza kuhatarisha nafasi za kazi .Ukweli ni kwamba bila ya mazingira hakuna uchumi. Mazingira kwa hivyo ndiyo yanayobidi kutangulizwa mbele katika mikakati yote siku za mbele."
Kitisho cha kudorora uchumi Ujerumani
Enzi za neema zinaashiria kutoweka nchini Ujerumani ambaako hiofu zimeenea kuhusu uwezekano wa uchumi kudorora. Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika: "Sekta zote zitalazimika kujirekebisha ili kuepusha balaa la kutoweka. Makampuni ambayo wakati mmoja yaliangaliwa kama kitambulisho cha neema nchini Ujerumani, yanabidi yabuni mfumo wa aina mpya. Hali hiyo inayahusu makampuni ya magari sawa na benki, mashirika ya bima na makampuni ya nishati. Mageuzi yanahitaji pia kuwepo waajiriwa wengine wenye ujuzi.Ujerumani inahitaji fikra mpya kwaajili ya wakati mgumu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga