1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hong Kong yasitisha kwa muda muswada kuhusu watuhumiwa

Yusra Buwayhid
15 Juni 2019

Kiongozi wa Hong Kong Jumamosi ameamua kusimamisha kwa muda muswada wa sheria wa kutaka wahalifu wa Hong Kong wapelekwe kushtakiwa China Bara, lakini waandamanaji wameahidi kuendelea na maandamano Jumapili.

https://p.dw.com/p/3KWas
Carrie Lam in HongKong
Picha: picture-alliance/Kyodo

 Muswada huo uliopendekezwa wa kutaka wahalifu wa Hong Kong wapelekwe kushtakiwa China Bara umesababisha mgawanyiko na machafuko yasiyo ya kawaida. Na uamuzi wa Carrie Lam wa kusimamisha muswada huo kwa muda umekataliwa mara moja na viongozi wa maandamano yanayoendelea kwa wiki nzima Hong Kong, ambao wamemtaka kiongozi huyo ajiuzulu, aufute muswada huo pamoja na kuuomba msamaha umma kwa mbinu za kikatili zilotumiwa na polisi wakati wa maandamano hayo.

Siku ya Jumatano jimbo la Hong Kong ambalo ni kitovu cha kifedha kimataifa lilishuhudia vurugu mbaya zaidi za kisiasa kuwahi kutokea tangu mwaka 1997, wakati eneo hilo liliporudishwa chini ya utawala wa China. Maelfu ya waandamanaji walitawanywa na polisi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi pamja na risasi za mpira.

Makabiliano hayo kati ya raia na polisi yalifanyika siku tatu baada ya Lam kukataa kubadilisha msimamo wake kuhusu muswada huo hata baada ya kufanyika maandamano makubwa yaliyovunja rekodi. Walioandaa maandamano hayo wamesema zaidi ya watu milioni moja waliandamana katika barabara za Hong Kong kupinga muswada huo unaoungwa mkono na serikali ya China. 

Wakosoaji wanaogopa sheria hiyo huenda ikwawatumbukiza watuhumiwa wa Hong Kong katika mahakama za China zinazoshawishiwa kisiasa pamoja na kuharibu sifa ya Hong Kong kama eneo salama kwa biashara.

Hongkong Protest gegen Auslieferungen nach China & Ausschreitungen
Waandamanaji Hong KongPicha: Reuters/T. Peter

Lam hana nia ya kujiuzulu

Hatua ya Lam kubadilisha msimamo wake ni ya nadra katika mji unaongozwa na viongozi wanaoelemea zaidi upande wa China Bara, ambao wamezoeleka kukataa madai ya waandamanaji wanaogombania demokrasia katika miaka ya hivi karibuni.

Lakini hasira kuhusu namna polisi na viongozi wa mji huo walivyowakandamiza waandamaanji hasa vijana bado inatokota, na wapinzani wa muswada huo wanatumai kujitokeza kwa idadi kubwa katika maandamano yajayo kutamzidishia shinikizo Lam.

Lakini Mtendaji Mkuu huyo -- ambaye anateuliwa na kamati yenye wajumbe wanaoiunga mkono serikali ya China-- kasema hana nia ya kujiuzulu.

"Ninasikitishwa kwamba mapungufu katika kazi yetu pamoja na sababu nyingine kadhaa yamesababisha utata na migogoro katika jamii kufuatia utulivu wa muda wa miaka miwili," amesema Lam.

China na Uingereza zaunga mkono uamuzi wa Hong Kong

Serikali ya China imesema Jumamosi kwamba inaunga mkono uamuzi wa kiongozi wa Hong Kong, kusitisha kwa muda muswada huo uliokosa uungwaji mkono na kusababisha maandamano ya wiki nzima, ambao unataka wahalifu wa Hong Kong wapelekwe kushtakiwa China Bara.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya China Geng Shuang ameualezea uamuzi huo kuwa ni hatua ya "kusikiliza kwa makini zaidi mitazamo ya jamii na kurejesha utulivu haraka iwezekanavyo."

Hongkong Protest gegen Auslieferungen nach China & Ausschreitungen
Maandamano ya umma Hong KongPicha: Reuters/A. Perawongmetha

"Tunaunga mkono, tunaheshimu na kuuelewa uamuzi huu," amesema Geng Shuang katika taarifa yake aliyoita masaa kadhaa baada ya Mtendaji Mkuu wa Hong Kong Carrie Lam kutangaza kusitishwa kwa muda muswada huo.

Taarifa tofauti na hiyo iliyotolewa na ofisi ya serikali kuu ya China ambayo inahusika na mambo yanayoihusu Hong Kong imesema muswada huo wa kutaka kuwasafirisha wahalifu wa Hong Kong kwenda kushitakiwa China bara ni 'muhimu na wa haki' katika kuziba kile ilichotaja kuwa pengo katika sheria za sasa.

Taarifa ya ofisi hiyo pia imesema China inaendelea kuunga mkono muswada huo, na inafuatilia kwa karibu upinzani wa umma dhidi ya muswada huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Jeremy Hunt ameupokea vizuri uamuzi huo wa serikali ya Hong Kong.

Uingereza iliirejesha Hong Kong chini ya utawala wa China mnamo mwaka 1997, kupitia mfumo wa 'nchi moja, mifumo miwili', ambao ulitegemewa kuhakikisha Hong Kong inapata uhuru wa kiwango cha juu ambao haupatikani pengine kokote nchini China.

Chanzo (rtre,afp,ap)