Homa ya uchaguzi wa 2022 yapanda Kenya
16 Aprili 2019Baadhi ya wabunge wa upande wa upinzani wanashinikiza wenzao wanaomuunga mkono Ruto kwenye harakati za kuwania urais mwaka 2022 kupigwa marufuku kuandaa mihadhara.
Wabunge hao wanane wanadai kwamba wafuasi hao wa Ruto wanazunguka wakitoa matamshi yasiyoridhisha, jambo linalorejesha nyuma juhudi za kuwa na umoja wa kitaifa zinazosukumwa na mwafaka uliofikiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.
Wakiwa bungeni, waliwakosoa wanaompinga Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, aliyesema kuwa makamu huyo wa rais hatakuwako kwenye mchakato wa kuwania urais mwaka 2022. Mmoja wa wabunge hao,
Babu Owino ambaye ni mbunge wa Embakasi Mashariki, alisema kuwa Atwoli "ni kiongozi wa jamii", huku mwenzake wa Alego Usonga, Samuel Atandi, akisema kuwa "kauli za Atwoli iinawazikilisha sauti ya Wakenya."
Atwoli aliyasema hayo akiwa mjini Lamu mwishoni mwa wiki, ambapo alitangaza pia kuunga mkono harakati za Gavana wa Kaunti ya Mombasa, Ali Hassan Joho, kuwania urais wakati huo.
Wafuasi wa Ruto wajipanga
Wakati huohuo, upande wa wanaomuunga mkono makamu wa rais nao wanajiandaa kwa mapambano.
Benjamin Washiali, kiranja wa bunge wa Jubilee anayemuunga mkono Ruto, aliweka bayana kuwa anaandaa mikakati ya kuwachukulia hatua wabunge ambao wanampinga Ruto na kwamba angelilifikisha hilo kwenye uongozi wa juu wa Jubilee.
Yote hayo yakiendelea, wafuasi wa Ruto walimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi, Hillary Mutyambai, kumuongezea ulinzi kiongozi huyo kwa sababu ya kauli kali zinazotolewa kupinga azma yake ya kuwania urais mwaka 2022.
Imetayarishwa na Thelma Mwadzaya, DW Nairobi