Hollerbach aachia ngazi Hamburg SV
12 Machi 2018
Ni timu ambayo haijashuka daraja tangu Bundesliga kuanzishwa mwaka 1963. Imekwisha kuwa bingwa wa ligi ya taifa Bundesliga mara 6, kombe la shirikisho DFB Pokal mara 3, kombe la washindi barani Ulaya, hivi sasa Europa League mara 1 na Kombe la Ulaya , hivi sasa Champions League mara 1. Timu hii ni Hamburger SV ambayo kwa jina la utani inaitwa Dino, ama Dinosaurus, wanyama waliokuwa wakiishi katika dunia miaka milioni kadhaa iliyopita ambao sasa hawako tena.
Hiyo ndio historia fupi ya Hamburg SV ambayo ni ya mafanikio makubwa katika soka la Ujerumani, timu ambayo aliichezea pia mchezaji maafuru wa Ujerumani Kaiza Franz Beckenbauear na mchezaji maarufu wa Uingereza Kevin Keegan. Lakini hivi sasa imo katika hatari ya kushuka daraja la pili na kumekuwa na mtafaruku mkubwa katika timu hiyo.
Misimu minne iliypopita Hamburg SV imebadilisha makocha zaidi ya kumi na hakuna hata mmoja aliyeonesha kuiletea uhai timu hiyo licha ya kuiokoa tu dhidi ya kushuka daraja. Lakini msimu huu hali inaonekana kuwa ngumu zaidi kwani Kocha Bernd Hollerbach aliyeteuliwa kuiokoa timu hiyo naye kibarua kimeota majani.
Leo Jumatatu(12.03.2018) kocha wa vijana wa umri chini ya miaka 21 wa klabu hiyo Christian Titz anatarajiwa kutajwa rasmi kuwa kocha wa timu ya kwanza.
Hatua ya kumuondoa Hollerbach imekuja baada ya kichapo cha mabo 6-0 dhidi ya mabingwa watarajiwa FC Bayern. Mchezaji wa Hamburg SV Sven Schipplock anasema:
"Hapa kwa kweli ni suala la kupambana tu, kama kuna uwezekano wa kushikilia matokeo ya 0-0 na nafasi chache zinazopatikana , kuzitumia. Lakini tulisambaratika baada ya dakika chache. Sifahamu , kichwani tunafikiria nini. Kwasababu hakuna anayeelewa, na mimi pia sifahamu."
Alipoulizwa mchezaji wa Bayern Munich Arjen Robben iwapo hawakuwahurumia wenzao wa Hamburg alisema:
"Nini maana ya kuhurumia ? Nafikiri , wao pia hawakuhitaji kuhurumiwa. Hii ni kandanda. Huo ndio ukweli, ambapo wanajikuta hivi sasa. Lakini sifikiri, kwamba tuliingia katika mchezo huo tukiwahurumia. Tunacheza mchezo wetu, tunashinda, tunahitaji kufunga mabao, tunahitaji kujisikia raha."
Bayern huenda ikatawazwa mabingwa mchezo wa 27
Bayern ambayo inaongoza Bundesliga kwa pointi 66 na timu inayoifuatia Schalke 04 ikiwa na pointi 46 huenda ikatawazwa mabingwa katika mchezo wa 27 ujao wakati itakapopambana dhidi ya RB Leipzig.
Schalke 04 wameng'ang'ania katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi baada ya kuishinda Mainz 05 kwa bao 1-0 siku ya Ijumaa. Lakini Borussia Dortmund ilipata changamoto kubwa kuweza kunyakua pointi zote tatu jana Jumapili baada ya kufanyakazi ya ziada kuishinda Eintracht Frankfurt kwa mabao 3-2 katika mchezo ambao timu zote ziliingia uwanjani zikiwa na pointi 42, zikiwania kushika nafasi ya tatu. Alikuwa Michy Batschuayi aliyeazimwa kutoka Chelsea aliyeipatia ushindi Dortmund baada ya kufunga bao la ushindi katika dakika ya 94 ya nyongeza. Nahodha wa Dortmund Marcel Schmelzer:
"Tumepoteza nafasi nyingi katika michezo yetu , kama vile dhidi ya Augsburg. Dhidi ya Leipzig tulicheza vizuri na timu ambayo ni washindani wa moja kwa moja. Leo pia Frankfurt wametupa changamoto kubwa, ilikuwa muhimu , kwamba katika mchezo huu wa pointi 6 tumeweza kupambana na kupata pointi 3 muhimu. Ni duru ngumu kabisa ya mwisho.
Leo hii timu inayokamata mkia katika Bundesliga FC Kolon inatapia maisha yake kwa kupambana na Werder Bremen. FC Kolon ina pointi 17 ikifuatiwa na Hamburg SV yenye pointi 18 na Kolon ikishinda leo jioni itajiweka katika nafasi nzuri ya kujinasua kutoka katika hatari ya kushuka daraka , ikiwa imesalia michezo 7 kabla ya Bundesliga kukunja janvi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman