1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande: Mapambano dhidi ya waasi wa Mali yafaulu

29 Januari 2013

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, amesema vikosi vya nchi yake na vya Afrika vinafaulu katika vita dhidi ya waasi wa Kiislamu nchini Mali, ingawa sasa anataka wanajeshi wa Afrika ndio wachukuwe jukumu la mbele zaidi.

https://p.dw.com/p/17TIz
France's President Francois Hollande delivers a statment on the situation in Mali at the Elysee Palace in Paris, January 11, 2013. France's President Hollande confirmed that French armed forces began an intervention today to support Malian government forces. REUTERS/Philippe Wojazer (FRANCE - Tags: POLITICS)
Frankreich militärische Unterstützung von Regierungstruppen in MaliPicha: Reuters

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Paris hapo jana, Hollande amesisitiza kuwa ni jukumu la wanajeshi wa Afrika kuikamilisha kazi ya kuikomboa kikamilifu Mali kutoka mikononi mwa waasi.

"Eneo la Mali kaskazini bado linadhibitiwa na magaidi. Kwa hiyo ni wajibu wa Waafrika kuisaidia Mali kuimarisha tena usalama na uhuru wa mipaka yake." Alisema Holande.

Kiongozi huyo aliyasema hayo wakati vikosi vya Mali vikisaidiwa na vya Ufaransa vilipoudhibiti mji wa kale wa Timbuktu. Wanajeshi hao sasa wanapania kuukomboa mji wa Kidal, karibu na mpaka na Algeria, ngome ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Ansar Dine.

Hollande ameeleza wazi kuwa kuudhibiti tena mji huo hakutakuwa na maana operesheni ya Ufaransa katika koloni lake hilo la zamani itakuwa imefikia tamati.

Ndege zisizo rubani karibu na Mali

Jeshi la Marekani linapanga kujenga kambi ya ndege zisizoendeshwa na rubani kaskazini magharibi mwa Afrika, karibu na Mali. Afisa wa Marekani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba lengo la kambi hiyo ni kuimarisha kazi ya kuyafuatilia makundi yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda katika eneo hilo na makundi mengine ya wanamgambo wa Kiislamu.

FILE - This Nov. 8, 2011 file photo shows a Predator B unmanned aircraft taxis at the Naval Air Station in Corpus Christi, Texas. The White House has no intentions to end CIA drone strikes against militant targets on Pakistani soil, setting the two countries up for diplomatic blows after Pakistani's parliament unanimously approved new guidelines for the country in its troubled relationship with the US, US and Pakistani officials say. (Foto:Eric Gay, File/AP/dapd)
Ndege zisizoendeshwa na rubaniPicha: dapd

Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kambi ya ndege hizo huenda ikajengwa nchini Niger, kwenye mpaka wa mashariki wa Mali, ambako wanajeshi wa Ufaransa wanafanya harakati dhidi ya kitengo cha al-Qaida katika eneo la maghreb (AQIM). Kambi hiyo itarahisisha ukusanyaji wa taarifa za kijasusi kutumia ndege zisizo na rubani kuhusu mienendo ya makundi hayo.

Kitisho cha mashambulizi ya kigaidi Ujerumani

Wakati huo huo, vyombo vya usalama vya Ujerumani vimeonya juu ya kuongezeka kitisho cha kufanyika mashambulizi ya kigaidi. Hofu hiyo inatokana na hatua ya serikali ya Ujerumani kupitia jeshi lake, Bundeswehr, kupeleka ndege za kusafirisha bidhaa na wanajeshi kusaidia mapambano dhidi ya waasi wa Mali.

Gazeti la Ujerumani, Bild, limeripoti kuwa hatua hiyo huenda ikachochea watu binafsi au makundi madogo kufanya mashambulizi ndani au nje ya Ujerumani.

Mali yapewa mkopo

Kwa upande mwingine, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeidhinisha mkopo wa thamani ya dola milioni 18.4 kwa ajili ya Mali. Bodi ya shirika hilo iliridhia mkopo huo hapo jana huku nchi hiyo ikijaribu kuondokana na athari zilizosababishwa na upinzani wa wanamgambo wa Kiislamu.

Mmoja wa wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali, ambako operesheni yao inatajwa kufanikiwa kuwashinda wanamgambo wa Kiislamu.
Mmoja wa wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali, ambako operesheni yao inatajwa kufanikiwa kuwashinda wanamgambo wa Kiislamu.Picha: picture-alliance/dpa

Shirika la IMF lilisitisha mkopo wa dola milioni 46.3 ulioidhinishwa mwaka 2011 kwa ajili ya Mali kufuatia mapinduzi ya kijeshi zaidi ya miezi tisa iliyopita. Mkopo huo ulinuiwa kutolewa kwa awamu hadi kufikia mwaka 2014.

Wafadhili wa kimataifa wanakutana leo nchini Ethiopia kuchanga fedha kukidhamini kikosi maalumu cha Afrika kwa ajili ya Mali, kitakachochukua nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa mara tu miji mikubwa itakapodhibitiwa. Umoja wa Ulaya umeahidi Euro milioni 50 kwa kikosi hicho, lakini sio kwa kununulia silaha.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE/AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba