1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande: Boko Haram bado ni kitisho kikubwa

Caro Robi14 Mei 2016

Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema Boko Haram bado ni kitisho licha ya hatua za kuridhisha za kijeshi zilizochukuliwa kuliangamiza kundi hilo la waasi lenya ngome yake nchini Nigeria.

https://p.dw.com/p/1Inuo
Picha: Reuters/A. Sotunde

Akizungumza katika mkutano wa kilele kujadili kitisho hicho cha Boko Haram mjini Abuja, Nigeria, Hollande amesema matokeo ya operesheni dhidi ya Boko Haram ni ya kuridhisha kwani waasi hao wamekatwa makali na kulazimika kurudi nyuma.

Nigeria ni mwenyeji wa mkutano huo wa kilele wa kujaidli kitisho kinachosababishwa na uasi huo wa Boko Haram, mkutano unaowaleta pamoja viongozi wa Ufaransa, Cameroon, Niger, Benin na Niger.

Na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philiph Hammond, naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken, maafisa wa jumuiya za Afrika magharibi na kati na maafisa wa Umoja wa Ulaya.

Miaka saba ya uasi kaskazini mashariki mwa Nigeria, imesababisha mauaji ya watu takriban 20,000 na kuwaacha wengine milioni 2.6 bila ya makaazi na kusababisha mzozo wa kibinadamu

Boko Haram ikabiliwe vipi?

Mazungumzo katika mkutano wa kilele wa usalama unatarajiwa kuangazia kutumwa rasmi kwa kikosi cha wanajeshi wa nchi za kanda hiyo ya magahraibi mwa Afrika kinachohusisha Nigeria na majirani zake kukabiliana na Boko Haram.

Rais wa Cameroon Paul Biya na Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari
Rais wa Cameroon Paul Biya na Rais wa Nigeria Muhamadu BuhariPicha: DW/Abuja

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake kuhusu mafungamano kati ya kundi hilo la Boko Haram na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS baada ya ripoti kuwa kuna wapiganaji wa kutoka Nigeria wanaopigana vita vya kijihadi Libya.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mafungamano hayo ni kitisho kwa usalama barani Afrika.

Baraza la usalama hapo jana Ijumaa limesema mazungumzo ya Abuja yanapaswa kuunda mkakati madhubuti wa kushughulikia uongozi, usalama, maendeleo na usaidizi wa kiuchumi, kijamii na kibinadamu kuushughulikia mzozo uliosababishwa na uasi wa Boko Haram katika kanda hiyo.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau mwaka jana alitangaza kuwa mtiifu kwa kiongozi wa IS Abu Bakr Al Baghdad. Ufaransa imetoa mafunzo na vifaa kama sehemu ya juhidi za kimataifa za kuisaidia Nigeria kukabiliana na Boko Haram. Hollande na Buhari wametia saini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili.

Hammond pia ameonya kuwepo kitisho kikubwa kutokana na mafungamano ya Boko Haram na IS lakini amesema kuna ufanisi katika kukabiliana na makundi hayo kufuatia usaidizi kutoka kwa Ufaransa, Uingereza na Marekani.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Uingereza amesema huu sio wakati wa kulegeza kamba katika vita dhidi ya Boko Haram na kuna haja ya kurejesha uthabiti katika kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mkutano huo wa kilele, unakuja miaka miwili baada ya mwingine wa ngazi ya juu kufanyika Paris. Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana vikali na waasi wa Boko Haram katika siku za hivi karibuni katika msitu wa Sambisa ambao ni ngome ya waasi hao.

Je Buhari atawaangamiza waasi?

Rais Buhari ameapa kulishinda kundi hilo kabla ya kumaliza mwaka mmoja tangu aingie madarakani. Jeshi la Nigeria limetangaza kundi hilo linasambaratika. Hata hivyo naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken amesema haionekani kama Boko Haram limeshindwa.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar ShekauPicha: picture alliance/AP Photo

Kutumwa kwa kikosi cha wanajeshi 8,500 wa kikanda kitakachojumuisha wanajeshi kutoka Nigeria, Benin, Cameroon, Chad na Niger kunatarajiwa kuwepo miongoni mwa ajenda kuu za mkutano huo.

Kikosi kinachoungwa mkono na Umoja wa Afrika kilicho na makao yake katika mji mkuu wa Chad, N'djamena kilipaswa kuanza kufanya operesheni dhidi ya Boko Haram mwezi Julai mwaka jana.

Boko Haram imetanua mashambulizi yake nje ya Nigeria, na mara kadha imezishambulia, Cameroon, Niger na Chad. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema watu milioni 9.2 katika nchi hizo wameathirika na mzozo huo.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Sudi Mnette