Hollande akutana na Abbas, aijia juu Iran
18 Novemba 2013Ziara ya siku tatu ya Rais Hollande kwenye eneo la Mashariki ya Kati, inasadifiana na kuanza tena kwa duru nyengine ya mazungumzo kati ya Iran na mataifa matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani, mjini Geneva, wiki ijayo.
Rais Shimon Peres na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wameelezea kufurahishwa kwao na ujio wa Hollande na namna Rais huyo wa Ufaransa alivyoshadidia msimamo wake mkali dhidi ya utawala wa Iran, ambao ni hasimu wa Netanyahu.
Akiwa mjini Tel-Aviv hapo jana, Hollande alitumia lugha ya Kihibru kusema kwamba anawapenda Mayahudi wote na kwamba historia yao inamfanya aone "umuhimu wa kuzuia mauaji mengine ya maangamizi dhidi yao", maarufu kama Holocast.
Akishadidia msimamo wa nchi yake kuelekea sera ya nyuklia ya Iran, Hollande alionya kwamba endapo Iran itaweza kupata silaha ya nyuklia, basi itakuwa "kitisho kwa Israel, eneo la mashariki ya kati na hata ulimwengu mzima" na kwamba ni wajibu wake kuzuia hilo lisitokee.
Fidia ya kushindwa kwa siasa za ndani?
Wachunguzi wa siasa za Mashariki ya Kati wanasema kwamba maneno haya ambayo yanakwendana mstari kwa mstari na yale ya Netanyahu dhidi ya Iran, huenda yamelengwa kuiimarisha taswira ya Hollande katika siasa za kimataifa kufidia kushindwa kwa siasa zake za ndani.
Ni Ufaransa inayotajwa kukwamisha duru ya kwanza ya mazungumzo ya mjini Geneva, kwa sababu ya kupigania kwake kile balozi mmoja wa Kimagharibi alichokiita "yasiyowezekana."
Netanyahu anayashutumu mataifa yanayojadiliana na Iran kwa kuwa kuzungumzia kile alichokiita "makubaliano mabaya" ambayo anadai yataipa Iran uwezo wa kutengeza vifaa vinavyohitajika kuunda bomu la nyuklia kwa siku 26 tu.
Netanyahu anatazamiwa kuzungumzia wasiwasi wake huo atakapokutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Moscow hapo Jumatano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, mjini Jerusalem hapo Ijumaa.
Leo (18 Novemba), Rais Hollande yuko kwenye Ukingo wa Magharibi kwa mazungumzo mafupi na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina, karibu na Ramallah.
Licha ya msimamo wake mkali dhidi ya Iran kwa maslahi ya Israel, Ufaransa inafahamika kwa msimamo wake unaoelemea Palestina panapohusika mzozo wa Mashariki ya Kati, na viongozi wa Palestina wanatarajia atachukua ujumbe wao kwa Israel, pale baadaye jioni ya leo atakapohutubia bunge la Israel, Knesset, mjini Jerusalem.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf