Hatari ya kuibuka upya kwa mapigano nchini Libya
13 Septemba 2016Vikosi hivyo ambavyo vilikabiliwa na upinzani mdogo wakati wakijaribu kutwaa bandari za Zuweitina, Ras Lanuf, Es Sider na Brega katika operesheni ambayo ilifanyika siku ya Jumapili, huku wakilazimisha kuondoka kwa wapinzani wao wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa huko Tripoli.
Mashambulizi hayo ni muendelezo wa kukusanya nguvu katika taifa hilo mwanachama wa Shirika la Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi, OPEC, miaka mitano baada ya kuangushwa kwa utawala wa Muammar Gaddafi na kutumbukia kwenye mapigano ambayo yameiacha nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika mgawanyiko wa makundi hasimu.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Jenerali Haftar juzi Jumapili inasema kuwa watazitunza bandari hizo kuhakikisha kuwa utendaji kazi wake unarudi mikononi mwa Shirika la Kusimalia Uzalishaji Mafuta la Libya, NOC, kuhakikisha kuwa hakutakuwa na aina yoyote ya kuingilia utendaji kazi katika uzalishaji.
Kitendo cha kutwaa bandari kinaiweka nchi hiyo katika hatari ya kuingia katika mgogoro mpya na pengine mataifa ya Magharibi yenye nguvu kuunda washirika hali ambayo inaweza kuchangia kuongeza kwa mgawanyiko baina yao.
Mwaka mmoja uliopita, Libya ilikuwa na serikali mbili hasimu, moja ni ile iliyoko Tripoli na nyingine ni ile iliyoko mashariki mwa nchi hiyo, huku serikali zote mbili zikiwa zinapigania udhibiti wa mafuta ambayo ni rasilimali ya kutegemewa nchini humo.
Hofu ya utawala unaoungwa mkono na Mataifa ya Magharibi
Mpango wa kuyaleta pamoja makundi hayo ambao ulisamimiwa na Umoja wa Mataifa ulitiwa saini mwezi Disemba, licha ya kuwa kulikuwa na upinzani kutoka kwa makundi ya watu wachache na tangu hapo baadhi ya vyama vya siasa na viongozi wa makabila kutoka upande wa Mashariki wamejizuia kushiriki wakihofia kuundwa kwa serikali mpya ya wapinzani ambayo inaungwa mkono na mataifa ya Magharibi.
Inaelezwa kuwa kunaweza kuwa na ugumu kutoka kwa wapinzani wa Haftar wa kufikia makubaliano kati ya jeshi na chombo kinachosimamia uzalishaji wa mafuta hali ambayo inaweza kuendeleza mgogoro nchini Libya.
Watu wengi mjini Tripoli na wale wa magharibi mwa nchi huyo wanamkosoa Haftar na kusema kuwa ni kiongozi anayejiandaa kutawala kidikteta licha ya kuwa anaonekana kuwa ni kiongozi wa kawaida kwa watu wengi wa mashariki mwa nchi ambao wanahisi kutelekezwa na Serikali ya mji mkuu.
Mapigano pamoja na mizozo ya kisiasa imeupunguzia Libya uwezo wa kuzalisha mafuta kwa kiwango kikubwa ambacho hakikuwahi kushuhudiwa kabla hali iliyosababisha kuondolewa kwa utawala wa Gaddafi miaka mitano iliyopita.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef