Hofu kama mkutano wa hali ya hewa utafanikiwa
17 Desemba 2009Maafisa nchini Denmark wamesema matumaini ya kupatikana Makubaliano ya kupambana na ujoto duniani, katika mkutano wa hali ya hewa huko Copenhagen, yanazidi kudidimia, siku moja kabla ya kilele cha mkutano huo wa siku 12. Mataifa yaliyoendelea na mataifa yanayoendelea yameshindwa kupata ufumbuzi wa kupunguzwa viwango vya gesi zinazochafua mazingira. Rais Barack Obama atawasili kesho mjini Copenhagen kuungana na viongozi wengine 120, huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akisema mambo sio mazuri, Copenhagen .
Hivyo ndivyo serikali ya Denmark mwenyeji wa mkutano wa hali ya hewa ilivyogusia - mambo si mazuri Copenhagen. Ulimwengu unakodolea macho kufeli kwa Viongozi wakuu wa dunia kupata ufumbuzi wa tishio kubwa la karne ya 21- mabadiliko ya hali ya hewa.
Na huku viongozi hao wakianza kumiminika Copenhagen- tayari wameanza kuashiria kuwa mkutano huo wa siku 12 utashindwa kufikia mkataba wowote wa kukabiliana na athari za ongezeko la hali ya ujoto duniani, kutokana na mivutano na utendaji- hasa kutoka kwa mataifa mawili yanayochafua zaidi hali ya hewa- Marekani na China.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumza mjini Berlin kabla ya kuelekea Copenhagen amesema malengo yaliyotolewa na mataifa tajiri kiviwanda huko Copenhagen si ya kuridhisha na kwamba mapendekezo ya Marekani hayatii moyo.
Mawaziri wa mazingira wameshindwa kukubaliana na rasimu itakayowasilishwa kwa viongozi hao kutia saini kwa sababu wameshindwa kuziba mwanya uliojitokeza- vipi mataifa yanayoendelea yataungana na mataifa tajiri duniani kupunguza gesi zinazoharibu mazingira.
Pendekezo la serikali ya Denmark mwenyeji wa mkutano huo, kwa mkutano huo kujigawa katika makundi madogo madogo ili kuharakisha majadiliano, lilipata pingamizi kali kutoka kwa mataida maskini yaliyoungwa mkono na China, nchi inayochafua zaidi hali ya hewa.
Duru za habari kutoka Copenhagen zinasema, mambo yamwekwama, hata majadiliano hayaonekani kupiga hatua yeyote. '' tunakabiliwana na tatizo kubwa'' alisema afisa mmoja kutoka Copenhagen. Na kuwasili kwa Waziri mkuu wa China Wen pamoja na Rais wa Brazil Lula Da Silva hivi leo kunatazamiwa kupiga jeki majadiliano hayo.
Rais Barack Obama ambaye nchi yake ni ya pili kwa kutoa gesi zinazochafua mazingira duniani , anatarajiwa kuwasili kesho Copenhagen na tayari amesema kuwa anataka makubaliano ambayo yanaweka hatua muhimu.
China , nchi inayochafua zaidi hali ya hewa, imezishtumu nchi za magharibi kwa kufanya ujanja na kujaribu kuilaumu kwa kushindwa kwa aina yoyote kwa mkutano wa Copenhagen kufikia makubaliano ya kupambana na kupanda kwa ujoto duniani.
Mvutano huu kati ya Marekani na China- umewatia wasiwasi viongozi wengi, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anaonya Copenhagen itafeli kutokana na kwamba Marekani na China hawajatoa malengo yanayotia moyo.
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso ametolea wito Marekani na China kufanya jitihada zaidi.
Baadhi ya viongozi wakuu watakaohutubia mkutano huo kuanzia leo ni pamoja na Rais Mahmoud Ahmedinejad, Kansela wa Ujerumani Angel Merkel , Rais Lula Da Silva na Rais wa Ufaransa Nichols Sarkozy.
Mwandishi: Munira Muhammad/ RTRE
Mhariri: Hamidou OummiKheir