1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoffenheim yakanyagwa vibaya na Mainz

25 Novemba 2019

Hoffenheim imekosa fursa ya kusonga hadi nafasi ya nne katika Bundesliga baada ya kupigwa mabao matano kwa moja dhidi ya Mainz ikicheza chini ya kocha mpya Achim Beierlorzer.

https://p.dw.com/p/3TgV1
Fußball Bundesliga | Hoffenheim vs Mainz
Picha: imago images/J. Huebner

Beierlorzer alifutwa kalamu na Cologne siku tisa kabla ya kuchukua usukani wa Mainz mnamo Novemba 18 na amesema ushindi wa mechi yake ya kwanza ni kwa heshima ya kocha aliyefutwa kalamu Sandro Schwarz.

Mapema jana, Hertha Berlin waliendelea kuyumba baada ya kunyukwa 4 – 0 dhidi ya Augsburg. Wamepoteza mechi yao ya tano mfululizo na kuanguka nyuma ya Ausgburg kwenye msimamo wa ligi.

Hapo jana, Jumapili, kikosi cha Borussia Dortmund kilizomewa na mashabiki wakati kikihudhuria mkutano wa kila mwaka wa klabu. Kocha wa klabu hiyo Lucien Favre yuko chini ya mbinyo baada ya timu yake kutoka sare na Paderborn Ijumaa. Na baada ya mechi hiyo, Michael Zorc, mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo alibaki mdomo wazi

Fußball Bundesliga | Training BV Borussia Dortmund |  Hans-Joachim Watzke und Trainer Lucien Favre
Lucien Favre anakabiliwa na mbinyo klabuniPicha: imago images/DeFodi

Tafadhali elewa kuwa sitosema mengi kwa sasa baada ya mechi hii. Kitu pekee ni kuwa kipindi cha kwanza tulicheza hovyo na haikubaliki na unapaswa kuomba radhi kwa mashabiki. kesho ni siku nyingine...

Dortmund ambayo ilipigiwa upatu na wengi kuwania taji msimu huu, ipo katika nafasi ya sita. Na wakati Dortmund wakionekana kuyumba, mahasimu wao Bayern Munich ambao hawana kocha wa kudumu kwa sasa, walipunguza pengo kileleni mwa ligi kwa pointi moja tu baada ya kuwakanyaga Fortuna Duesseldorf 4 – 0 wakati nao viongozi wa ligi Borussia Moenchengladbach wakipoteza 2 – 0 dhidi ya Union Berlin. Thomas Muller ni miongoni mwa wachezaji wanaoonekana kupata uhai tena katika Bayern hii mpya, na hapa anazungumzia mtannage ulivyokuwa

Ukilinganisha na ushindi wa 4 - 0 dhidi ya Dortmund, hii leo ilikuwa tu ni kurejesha hali yetu ya kawaida. Hakika, leo ilikuwa vigumu kiasi kwetu kiakili kuona kama kweli tunafanya vitu anavyovitaka kocha. Na nadhani tulidhihirisha hilo vizuri kabisa, hasa katika kipindi cha kwanza. Tumeridhika bila shaka.

Bayern wako nafasi ya tatu pointi 24 sawa na RB Leipzig ambao walipata ushindi wa 4 – 1 dhidi ya Cologne ambao walicheza mechi yao ya kwanza chini ya kocha mpya Markus Gisdol. Leipzig ni miongoni mwa timu zinazoonekana kuleta ushindani mkali msimu huu chini ya kocha wao chipukizi Julian Nagelsmann. Msikilize mchezaji Emil Forsberg

Inapendeza sana. Nadhani tulikuwa na mchezo mzuri. bila shaka tulipunguza kasi baada ya mapumziko lakini tulilinda vyema lango letu. Ni ushindi uliostahiki. Watu wengi walionyesha ari na kujiamini baada ya mechi za kimataifa. Hilo ni bora pia kwa timu. Na tutaendelea hivyo.