Historia ya Afghanistan na mazungumzo ya amani na Taliban
9 Juni 2018Kwa muda mrefu kundi la Taliban limesisitiza juu ya kuondolewa kabisa kwa majeshi yote ya kigeni kutoka Afghanistan kama sharti la kufanyika kwa mzungumzo -- kikwazo kikuu katika kuanzisha uwezekano wowote wa mazungumzo. Haya ni baadhi ya majaribio yaliyopita ya amani wakati wa uasi wa muda mrefu nchini humo.
Jeshi la Marekani liliivamia Afghanistan Oktoba 7, 2001, kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 yaliodaiwa kufanywa na kundi la Al-Qaeda, na kuliondoa madarakani kundi la Taliban katika muda wa wiki kadhaa. Lakini kufikia mwaka 2003, Marekani ilihamishia nadhari nchini Iraq.
Taliban na makundi mengine ya Kiislamu yakarudi nyuma kwenye ngome zao kusini na mashariki mwa Afghanistan, ambako waliweza kusafiria kwa urahisi kwenda na kutoka eneo la Pakistan lenye mamlaka yake ya ndani. Taratibu walianza kujikusanya upya.
Februari 2007 waasi wa Taliban walishambulia kituo cha jeshi la Marekani nchini Afghanistan, wakati makamu wa rais Dick Cheney akiwa ziarani nchini humo, na kuuwa 24.
Kilele cha wanajeshi wa NATO na kuuawa kwa Osama bin Laden
Rais wa Marekani Barack Obama aliamuru kuongezwa wanajeshi 30,000 zaidi nchini Afghanistan Desemba 2009, lakini akasema uondoaji utaanza Julai 2011. Idadi ya wanajeshi wa jumuiya ya kujihami ya NATO ikaongezeka na kufikia kilele cha wanajeshi 150,000 katika msimu wa joto mwaka 2010.
Hatimaye Mei 2011 kiongozi wa kundi la Al-Qaeda Osama bin Laden aliuawa na vikosi maalumu vya Marekani nchini Pakistan. Mauaji hayo yakapelekea miito ya kukomeshwa kwa vita hivyo. Muda mfupi baadae, Obama alitangaza kwamba wanajeshi 33,000 wa Marekani wataondolewa kufikia katikati mwaka 2012.
Mauaji ya mjumbe wa amani wa rais
Lakini matumaini ya mazungumzo yalififia wakati Burhanuddin Rabbani --- rais wa zamani na wakati huo mjumbe wa amani wa Rais Hamid Karzai -- alipouawa na kuwa mwanasiasa wa kwanza wa juu zaidi kuuawa katika mgogoro huo, katika mauaji ya Septemba 2011 ambayo maafisa wa serikali ya Afghanistan waliyalaumu kwa kundi la Taliban.
Juni 2013, Taliban walifungua ofisi nchini Qatar, kufuatia majadiliano ya siri na maafisa wa Marekani katika hatua ya kwanza kuelekea uwezekano wa makubaliano ya amani. Lakini mkakati huo ulivunjika mwezi mmoja baadae, baada ya ofisi hiyo kumkasirisha Karzai kwa kujitaja kuwa ubalozi usiyo rasmi wa serikali ilioko uhamishoni.
Desemba 2014, NATO ilihitimisha rasmi ujumbe wake wa mapambano nchini Afghanistan, na kukabidhi jukumu la kulinda usalama kwa vikosi dhaifu vya Afghanistan vilivyokuwa vinakabiliana na idadi inayoongezeka ya vifo na utoro.
Ufichuzi wa kifo cha Mullah Omar na kuibuka kwa IS
Lakini matumaini yakaongezeka tena wakati mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Kabul na Wataliban wa Afghanistan -- ya kwanza ya mgogoro huo -- yalipoanza nchini Pakistan Julai 2015. Ufichuzi wa kushtua kwamba Mullah Omar, mwasisi wa Taliban, alikuwa amefariki miaka miwili iliopita, na kwamba kundi hilo lilificha kifo chake, ukakwamisha haraka mazungumzo hayo.
Katika mwaka uliofuata, hali ya usalama ilizorota nchini Afghanistan, hasa mjini Kabul, huku kundi changa la Dola la Kiislamu likiongezea changamoto zinazovikabili vikosi vya usalama vya serikali. Mji huo mkuu ukageuka eneo hatari zaidi kwa maisha ya raia wakati idadi ya wahanga ikizidi kupanda.
Mwezi Februari mwaka huu wa 2018, Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani alizindua mpango wa kuanzisha mazungumzo na Taliban, ikiwemo hatimaye kulitambua kama chama cha siasa. Alipendekeza usitishaji mapigano kama sehemu ya mpango huo.
Ndiyo mpango mpana zaidi wa amani uliopendekezwa na serikali mjini Kabul, lakini ulikataliwa na Taliban, wanaoitazama serikali ya Ghani kama haramu, na badala yake waliongeza mashambulizi.
Hatua za 'kujenga imani' kati ya pande mbili
Mei 31 wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon ikasema maafisa wa Afghanistan wanajadiliana na Wataliban kuhusu usitishaji mapigano. Siku kadhaa baadae, Juni 7, Ghani akatangaza kilichoonekana kama mpango wa usitishaji mapigano wa upande mmoja na Taliban ili kutoa fursa ya kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr kwa amani, ingawa alisema operesheni dhidi ya makundi mengine likuwemo la Dola la Kiislamu zingeendelea.
Taliban hawakujibu mara moja, na wachambuzi wakaonyesha mashaka, wakati mitandao ya kijamii ikifurika na ujumbe unaowataka Wataliban wakubali. Maafisa wa NATO na Marekani wanasema wanatumai hatua hiyo itapelekea mafanikio.
Kufikia siku ya Jumamosi kundi la Taliban lilitangaza mpango wao wa kihitoria wa kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu za kwanza za Eid. Taarifa yao haikuwa inamjibu moja kwa moja Ghani, lakini tarehe zinagongana.
Hatua hizo zimepokelewa kwa tahadhari na wengi, lakini pia ni ahueni kwa raia na maafisa wa serikali ya Afghanistan waliochohwa na vita. Mchambuzi wa kimagharibi alieko mjini Kabul, aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kwamba hatua hizo ni za "kujenga imani."
Lakini suala la iwapo zinapelekea kufikiwa jambi kubwa zaidi bado haliwezi kusemwa kwa uhakika mapaka sasa.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/Afpe
Mhariri: Zainab Aziz