Hisia ya kubaguliwa na hofu
5 Desemba 2014Kuzuka na kusambaa kwa haraka kwa Ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi kulizua hofu na dhana ya kubaguliwa kwa waathiriwa, ambayo ni makosa.
Dhana: Endapo nitakutana na muathiriwa wa Ebola, bila shaka nitaambukizwa?
Jibu: Hapana. Virusi vya Ebola haviwezi kusambazwa kupitia hewa. Vinaweza tu kusambazwa kwa kushika damu au maji maji ya mtu aliyeambukizwa virusi vya Ebola. Kutokana na watu wengi kuwa na mazoe ya kutazama filamu za kutisha,, habari kwamba Ebola ni hatari zinasambaa kwa haraka sana. Lakini licha ya kwamba maelfu ya watu wamefariki kutokana na ugonjwa huu, virusi vinavyosababisha magonjwa mengine kama vile homa, husambaa haraka zaidi
Dhana: Vita dhidi ya Ebola haviwezi kushindwa
Jibu: Wataalamu wengi wanakubaliana kwamba kuzuka na kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola kunaweza kudhibitiwa kupitia juhudi za pamoja za jamii ya kimataifa, ingawa juhudi hizi huenda zitachukua muda wa miezi michache. Tayari kuna dawa ambazo zinaendelea kufanyiwa majaribio na huenda hivi karibuni zikaanza kutumika.
Dhana: Mataifa ya Magharibi ndiyo yaliyotengeneza Virusi vya Ebola
Jibu: Hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha dhana hii. Ugonjwa wa Ebola uligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo mwaka wa 1976 na mtafiti mmoja wa kisayansi kutoka Ulaya, lakini watafiti wanaamini kuwa virusi vya Ebola vimekuwepo kwa muda mrefu hata kabla ya kugunduliwa kwake katika msitu mkubwa wa taifa hilo la Afrika ya Kati na maeneo ya kusini mashariki mwa Asia.
Dhana: Ebola inaweza kutibiwa
Jibu: Hadi kufikia sasa hakuna dawa kwa uhakika ambayo inaweza kutibu ugonjwa wa Ebola. Ugonjwa huu unaweza tu kudhibitiwa kupitia tiba dhidi ya magonjwa mengine ambayo ni dalili au vyanzo vya ugonjwa huu. Kuna dawa ambazo kwa sasa zinaendelea kufanyiwa majaribio ili kutibu Ebola moja kwa moja. Kumekuwepo na Watu wanaoamini miujiza kwamba wanaweza kutibu Ugonjwa huu, lakini mbinu hizi ni hatari sana. Zaidi ya watu 400 walifariki nchini Sierra Leone baada ya mganga wa kudai kwamba anaweza kutibu Ebola, hali iliyofanya ugonjwa huu kusambaa kwa haraka.