1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisia mseto nchini Tanzania kuhusu CAG mpya, kwanini?

George Njogopa 5 Novemba 2019

Nchini Tanzania kuna matarajio yanayotofautiana kuhusu ujio wa Mdhibiti na Mkaguzi mpya wa hesabu za serikali(CAG) Charles Kichere aliyeanza kazi siku ya Jumanne baada ya kuapishwa na rais John Magufuli.

https://p.dw.com/p/3SV53
Tansania Dar es Salaam Vereidigung Controller Auditor General CAG
Picha: DW/ Eric Boniphace

Hatua hiyo inafuatia namna alivyopanda na kushuka katika ofisi nyingi za umma, na tukio la hivi karibuni kabisa ni la kuondolewa katika nafasi ya kamishna wa mamlaka ya mapato TRA na kupelekwa hadi nafasi ya chini ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe kabla ya sasa kurejeshwa kwenye nafasi nyingine ya juu

Mdhibiti na Mkaguzi mpya wa hesabu za serikali(CAG) nchini Tanzania Charles Kichere, ambaye ameanza kazi rasmi siku ya Jumanne anajukumu la kujitambulisha upya kwa wananchi namna anavyoweza kukivusha chombo hicho kinachotazamwa kama jicho la umma katika kumulika mwenendo wa matumizi ya serikali.

Mara zote ripoti zinazotolewa na ofisi hiyo imekuwa ikibaini maovu ya matumizi mabaya ya fedha za umma, na kwa maana hiyo Kichere anaingia katika wadhifa huo huku akijua hilo na ndiyo maana moja ya vipaumbele vyake vya mwanzo alivyobainisha na kukabiliana na wale wanaozifuja fedha za umma.

Tansania Dar es Salaam Vereidigung Controller Auditor General CAG
Rais Magufuli na CAG mpya Charles KicherePicha: DW/ Eric Boniphace

"Sitokuwa na subra na watu ambao wanatumia mapato ya serikali, nitawaripoti ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa", alisema Kichere.    

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, Kichere atapaswa kuchanga vyema karata zake hasa kwa kuzingatia kwamba ripoti nyingi zilizowahi kutolewa na ofisi hiyo zilibaini madudu ya uvujaji wa mali ya umma, huku halmashauri kadhaa zikipata hati chafu.

Pamoja na ripoti hizo kutoa mapendekezo mengi yaliyotaka wahusika wa vitendo hivyo kuchukuliwa hatua, ni mara chache hilo lilishuhudiwa kutendeka.

Mzozo ulioibuka baina ya Spika wa Bunge na CAG aliyemaliza muda wake, Professa Mussa Assad unatajwa ni moja ya ya chagizo lilitokana na namna ofisi hiyo ya mdhibiti ilivyotaka kuona masuala yaliyoibuliwa katika ripoti yakishughulikiwa kikamilifu.

Kichere ameahidi kuendelea kushirikiana na Bunge katika kutekeleza majukumu yake na kwamba hilo atalifanya kwa kusaidiana na watendaji wake.

" Tutaendeleza mahusiano mazuri kulikuwa na kuregarega baina ya mahusiano ya bunge na CAG"

Hata hivyo, wadadisi wanasema kwamba huenda mteule huyo mpya akajikuta akirudia kuchapisha ripoti zitakazofanana na watangulizi wake hatua ambayo inaweza kukwaza utendaji wake kama atashindwa kujitokeza hadharani na kukemea matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mtangulizi wake anatajwa kuwa ni mmoja ya wadhibiti aliyekuwa na uthubutu na wakati wote hakusita kutoa maoni yake pale alipoona yale aliyoyawasilisha kwenye ripoti zake yakisuasua kuchukuliwa maamuzi.

Tansania Parlament in Dar es Salaam | Job Ndugai, Sprecher
Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai Picha: DW/E. Boniphace

Kuondoka kwa CAG Assad kunafuatia kukamilika kipindi chake cha miaka mitano, ingawa wengi walidhania pengine angeongezewa kipindi kingine kama ilivyozoeleka kwa wengine waliomtangulia.

Kumekuwa na maoni mengi yanayodadisi kwa nini CAG Assad hakuongezewa muda, lakini akichambua sheria inayohusu ukaguzi wa umma ya mwaka 2008, wakili Leonard Manyama amewakosoa wale wanaoendeleza mjadala huo.

CAG Kichere anakuwa mdhibiti wa saba kushika wadhifa huo tangu Tanzania ipate uhuru huku CAG wa kwanza aliyetambulika kwa jina la McColl akidumu kwa kipindi cha miaka miwili.