1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisbollah yatoa mwito uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ususiwe

Mohamed Dahman29 Oktoba 2010

Mkuu wa wanamgambo wa kishiya nchini Libnan,Nasrullah amewatolea mwito walibnan kwa jumla wasusie uchunguzi wa Umoja wea mataifa kuhusu mauwaji ya waziri mkuu wa zamani Rafik Hariri

https://p.dw.com/p/Pu1k
Mkuu wa wanamgambo wa Hisbollah Sayyed Hassan NasrallahPicha: picture-alliance/dpa

Lebanon inakabiliwa na mzozo mpya wa kisiasa baada ya Hezbollah kutoa wito wa kususia mahakama inaoyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayochunguza mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri. Umoja wa Mataifa umeonya kwamba Lebanon imeingia katika hatari kubwa.

Hassan Nasrallah kiongozi wa chama cha wanamgambo wa Kishia hapo jana ametowa wito kwa wananchi wote wa Lebanon kuacha kutowa ushirikiano wao kwa wapelelezi wanaochunguza mauaji ya mwaka 2005 ya waziri mkuu huyo wa zamani na kuwaonya raia halikadhalika wanasiasa kwamba kuendelea kutowa ushirikiano wao itakuwa ni sawa na kukishambulia chama chake cha Hezbollah.

Onyo lake linazidi kumfarakisha na Waziri Mkuu wa madhehebu ya Sunni Saad Hariri ambaye ni mtoto wa kiume wa waziri mkuu huyo wa zamani aliyeuwawa, ambaye ameapa kuhakikisha kwamba uchunguzi huo unakamilika.Matamshi yake pia yamezusha hofu kwamba serikali ya Lebanon ilioundwa kwa tabu huenda ikasambaratika.

Waziri Mkuu mwenyewe binafsi bado hakutamka kitu juu ya wito huo wa Nasrallah ambaye mara kwa mara amekuwa akisema kwamba anatarajia chama chake kinachoungwa mkono na Iran na Syria kitatuhumiwa kuhusika na mauaji hayo jambo ambalo amesema litasababisha madhara ambayo hayakuyatolea ufafanuzi.

Ahmed Fatfat mbunge wa chama cha waziri mkuu cha Future Movement kinachoungwa mkono na Saudi Arabia na mataifa ya magharibi amesema waziri mkuu alikuwa akitarajiwa kuongoza mkutano wa chame chake leo hii lakini bado jambo hilo halikuthibitishwa.

Saad Hariri Sohn des ehemaligen Ministerpräsidenten des Libanons
Saad Hariri,waziri mkuu na mtoto wa waziri mkuu aliyeuliwa Rafik HaririPicha: AP

Fatfat amesema wito wa Nasrallah ni sawa na wito wa kutaka kuiasi jumuiya ya kimataifa na ameitaka serikali kuelezea msimamo wake juu ya kauli hiyo ya Nasrallah na iwapo inatengua sera ya serikali ambayo inasema kwamba inaheshimu na kuahidi kushirikiana na Mahkama Maalum kuhusu Lebanon.

Kiongozi wa Kikristo Samir Geagea ambapo chama chake cha Lebanese Forces ni washirika muhimu wa Hariri amewataka rais na waziri mkuu kuitisha mkutano wa dharura juu ya suala hilo.

Amesema hilo ni tishio kwa serikali ya Lebanon ambayo kama serikali kwanza inatakiwa itowe ushirikiano wake kwa wachunguzi kwa kupitia muongozo wa maelewano na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mahkama Maalum kwa ajili ya Lebanon yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi iliopewa majukumu ya kuchunguza kuuwawa kwa Hariri na watu wengine 22 kwa miripuko ya mabomu imelaani wito huo wa Nasrallah kuwa ni jaribio la kuzuwiya haki isitendeke.

Hali ya mvutano imekuwa ikiongezeka nchini Lebanon kutokana na repoti kwamba mahkama hiyo ya kimataifa itainyoshea kidole Hezbollah kwa kuhusika katika muaji ya Hariri.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mpitiaji: Josephat Charo