Hillary Clinton ahudhuria mkutano wake wa kwanza na mawaziri wa NATO.
5 Machi 2009Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton ametoa wito leo kwa jumuiya ya NATO na Urusi kuwa na mwanzo mpya kuhusiana na uhusiano wa pande hizo mbili, licha ya kusema kuwa jumuiya hiyo inapaswa kuweka mlango wazi kwa ajili ya uanachama wa majimbo ya zamani ya iliyokuwa Urusi ya Georgia na Ukraine.
Mawaziri wa jumuiya ya kujihami ya NATO walionekana kuunga mkono kuanza tena kwa mahusiano rasmi na Urusi, yaliyositishwa baada ya jeshi lake kuingia nchini Georgia August mwaka jana, katika haja ya kuundwa kwa nguvu kubwa zaidi dhidi ya wapiganaji nchini Afghanistan pamoja na vitisho vingine.
Muda umefika sasa wa mwanzo mpya. Tunaweza na tunapaswa kutafuta njia ili kuweza kufanyakazi vizuri na Urusi pale ambapo tuna maslahi ya pamoja , ikiwa ni pamoja na kuwasaidia watu wa Afghanistan , Clinton amesema katika mkutano wake wa kwanza wa ngazi ya juu wa jumuiya hiyo yenye wanachama 26.
Matamshi ya Clinton yanakwenda sambamba na mawazo ya utawala wa rais Barack Obama kuwa wakati umefika sasa wa kubonyeza kitufe cha kuanza upya na kufungua ukurasa mpya katika mahusiano na Urusi.
Clinton na washirika wengine wamesisitiza kuwa tofauti zinaendelea kuwapo na Urusi, hususan kuhusiana na Georgia. Lakini ameongeza kuwa NATO inapaswa kutafuta njia ya kushughulikia tofauti hizo wakati huo huo ikisisitiza misingi yake iwapo usalama ama maslahi yake yako hatarini.
Tunapaswa kuendelea kufungua milango ya NATO kwa nchi za Ulaya kama Georgia na Ukraine na kuwasaidia kufikia viwango vya NATO, Clinton amesema katika maelezo yaliyoandaliwa kabla.
Urusi inapinga uanachama wa NATO kwa mataifa hayo mawili yaliyokuwa majimbo ya zamani ya iliyokuwa Soviet Union kwa sababu inahofia kukaribiana sana na jumuiya hiyo ya kujihami katika eneo lake.
Utawala wa rais wa zamani wa Marekani George W. Bush umeongoza kusitishwa kwa majadiliano ndani ya baraza la pamoja kati ya NATO na Urusi , ambalo linaelekeza ushirikiano kuhusu masuala ya kiusalama kati ya pande hizo mbili, baada ya jeshi la Urusi kuingia nchini Georgia August mwaka jana.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza David Miliband amesema kuwa ufufuaji wa mahusiano hayo kati ya NATO na Urusi hivi sasa ni njia ya kupambana moja kwa moja na wasi wasi uliopo.
Katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer amesema kuwa ni dhahiri kuwa tuna maslahi ya pamoja na Urusi, haya ikiwa ni kupambana na ugaidi nchini Afghanistan, mapambano dhidi ya kusambaa kwa silaha za maangamizi na mengineyo.
Ameongeza kuwa hatusemi kuwa hakuna tofauti kubwa za mawazo ambazo bado zipo baina ya NATO na Urusi hususan kuhusu Georgia.
Nae waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema sasa kuna hali tofauti ya ushirikiano katika NATO.
Tunaweza kusema kuwa sasa unavuma upepo mpya katika NATO, na pia ninamatumaini kuwa kuna hali mpya ya ushirikiano , ambao tunauhitaji na kazi yetu itakuwa rahisi zaidi.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton pia amekuwa akitoa kwa washirika wa NATO picha ya hatua zilizopigwa katika mkakati wa rais Obama kuelekea Afghanistan na kuwataka washirika kutoa mawazo yao kuhusu njia bora zaidi za kuishughulikia hali inayozidi kuwa mbaya katika mapambano na wapiganaji wa Taliban.
Sekione Kitojo / RTRE