Hilary Clinton kuanza kampeni ya uchaguzi
22 Januari 2007Kuhusu kampeni ya uchaguzi ya Wademokrats wa Marekani, gazeti la “Handelsblatt” la mjini Düsseldorf lina haya ya kusema:
“Sababu ya Hilary Clinton kutangaza mapema kuwa anataka kugombea kiti cha rais ni Barack Obama. Mbunge huyu wa baraza la Senate tayari wiki moja iliyopita aliarifu mpango wake wa kutaka kugombea urais. Kwa hivyo ilimbidi Hilary Clinton kuchukua hatua hii haraka, ili asibaki nyuma katika shindano hili.”
Gazeti la “Märkische Oderzeitung” la mjini Frankfurt linakumbusha msimamo wa Clinton kuhusu vita vya Irak na linaandika:
“Shindano hili pia litafichua makosa ya Hilary Clinton. Mwanasiasa huyu aliviunga mkono vita vya Irak kwa nguvu na kubadilisha msimamo wake tu baada ya vita hivi kugeuka msiba. Akipinga sasa mkakati wa rais Bush kuongeza idadi ya wanajeshi huko Iraq, Clinton anaingia katika hatari ya kukosolewa vikali.”
Na hatimaye kuhusu suala hilo ni gazeti la “Leipziger Volkszeitung” ambalo limeandika yafuatayo:
“Suali la kusisimua kwenye uchaguzi huu si kama Wamarekani wako tayari kutawaliwa na mwanamke, bali ni kama wako tayari kutawaliwa tena na ukoo wa Clinton. Kwani licha ya rais wa zamani, Bill Clinton, kuonyesha kwamba anajizuia kujiingiza katika mambo ya siasa, hatuamini kuwa Clinton atafanya kazi za nyumbani tu.”
Mada nyingine inayozungumziwa na wahariri wa humu nchini ni kesi ya Murat Kurnaz, Mjerumani wa asili ya Kituruki aliyefungwa katika gereza ya Guantamano na sasa kuishtaki serikali ya Ujerumani kwa kuchelewa kumrudisha nyumbani kwa miaka kadhaa. Anayekosolewa hasa katika kesi hiyo ni waziri wa nchi za nje wa Ujerumani, Franz-Walter Steinmeier. Gazeti la “Abendzeitung” la kutoka Munich lina wasiwasi juu ya mustakabali wa Steinmeiner. Gazeti limeandika:
“Waziri Steinmeier anafanya kazi yake vizuri. Anaiwakilisha Ujerumani kwa njia ya kuaminika na kuheshimika. Kwa hivyo ni mbaya mno ikiwa alifanya kosa katika kesi hiyo ya Murat Kurnaz. Baada ya kufungwa kwa mwaka mmoja tu, maafisa wa Marekani walikubali kuwa Kurnaz si gaidi. Uamuzi huu ni wa kustaajabisha tukikumbuka kuwa mara nyingine Wamarekani wanatoa sababu zisizofahamika ili wasimuache huru gaidi mtuhumiwa. Iwapo kweli Steinmeier alizuia Kurnaz asirejeshwe Ujerumani, mustakabali wake kama waziri uko hatarini.”