Hilary Clinton ateuliwa kuwa Waziri wa mambo ya kigeni
2 Desemba 2008Chini ya mpango huo Waziri wa Ulinzi Robert Gates anaendelea kushika wadhifa huo.
Bi Clinton na Bwana Obama wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu masuala ya sera za kigeni na ulinzi nchini humo ila kwa sasa watashirikiana kubadili sura ya Marekani katika nchi za kigeni vilevile usimamizi katika vita kwenye mataifa ya Iraq na Afghanistan.
Rais mteule Barack Obama alipuuza tofauti zao na kusisitiza anaunga mkono mjadala katika kikosi chake kipya na kumsifu Bi Clinton.
Bwana Obama alisisitiza kuwa ana imani vikosi vya Marekani vitaondoka nchini Iraq katika kipindi cha miezi 16 punde baada ya kuapishwa.Hata hivyo alieleza kuwa atashauriana na wadau wakuu kuhusu suala hilo.Kadhalika Bwana Obama aliwateua Jenerali mstaafu James Jones kuwa mshauri mkuu wa kitaifa na Gavana wa Arizona Janet Napolitano kuwa mkuu wa idara ya usalama wa kitaifa.
Afisa wa masuala ya kisheria wa zamani Eric Holder naye ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu na Susan Rice aliyekuwa mshauri wa masuala ya kigeni ameteuliwa kuwa balozi katika Umoja wa mataifa.Wadhifa huo umepangwa kuorodheshwa katika Baraza la Mawaziri.
Wateule hao wanasubiri kuidhinishwa na Baraza la wawakilishi,Senate bila pingamizi zozote.