1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Herzog: Kusawazisha mahusiano na Saudia ni muhimu

18 Januari 2024

Rais wa Israel Isaac Herzog amesema kusawazisha mahusiano kati ya nchi yake na Saudi Arabia ni hatua muhimu ya kuvimaliza vita vyake dhidi ya Hamas.

https://p.dw.com/p/4bR2p
Isaac Herzog rais wa Israel
Rais wa Israel Isaac HerzogPicha: Heinz-Peter Bader/AP/picture alliance

Herzog ameyasema haya leo katika Kongamano la Kiuchumi Duniani linalofanyika huko Davos nchini Uswisi.

Rais huyo wa Israel amedai kuwa hatua hiyo itakuwa muhimu pia katika kubadilisha hali ya mambo katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati. 

"Muktadha wa kikanda ni muhimili muhimu wa ustawi na maendeleo. Ni muhimili wa upeo mzuri wa siku zijazo kwa kila anayehusika. Na kwa kweli chaguo la Saudia kama sehemu yake katika mchakato wa kusawazisha mambo, ni muhimu kwa kujiondoa kutoka kwenye vita na kuelekea katika upeo mpya. Hali bado si rahisi, itachukua muda ila nafikiri hii ni fursa ya kusonga mbele kikanda kwa ajili ya mustakabali mwema," alisema Herzog.

Jukwaa la Uchumi Duniani la Davos kuanza leo

Haya yanakuja siku kadhaa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan kusema katika mkutano huo kwamba, nchi hiyo ya kifalme inakiri kwamba amani ya kikanda inajumuisha amani ya Israel.

Faisal lakini aliongeza kwamba hilo litafanyika tu kupitia amani kwa Wapalestina, kupitia taifa la Palestina.