1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Helikopta za Uganda zapotea

13 Agosti 2012

Helikopta tatu za Uganda zikiwa njiani kuelekea Somalia zimepotea katika ardhi ya Kenya. Maafisa wa jeshi la Kenya wamesema leo kwamba helikopta nne ziliondoka Uganda na moja ikatuwa mjini Garissa.

https://p.dw.com/p/15ob3
Ndege ya kijeshi
Ndege ya kijeshiPicha: klix.ba

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Kenya Bogita Ongeri, helikopta hizo zilipotea karibu na eneo la mlima Kenya, lakini rubani mmoja aliweza kuwasiliana nao, akiomba msaada.Kwa mujibu wa msemaji huyo, mvua na hali mbaya ya hewa zilihujumu juhudi za uokozi na Ongeri akaongeza kwamba kundi la waokowaji limepelekwa sehemu hiyo ya ajali. Hata hivyo alisema hawafahamu kwa uhakika ni wapi hasa ajali hiyo ilitokea kwa sababu bado hali ya hewa ni mbaya. Helikopta hizo aina ya Mi-24 zinauwezo wa kubeba hadi abiria wanane.

Helikopta hizo ambazo ziliondoka Uganda jana, zinahofiwa kuwa zimeanguka kwenye eneo moja la milima lililojaa misitu, karibu na mlima wenye theluji wa Kenya na ambao una urefu wa mita 5,199. Mkuu wa Polisi wa mkoa Francis Munyambu amesema taarifa walizonazo ni kwamba kuna mahala mahsusi ambapo inaaminiwa ndiko kulikotokea ajali hiyo.Aidha Mbali na helikopta za kivita M-24 Uganda inaripotiwa pia kupeleka Somali ndege za uchukuzi zilizotengenezwa Urusi aina ya Mi-17.

Umoja wa Afrika wapanga kushambulia Kismayu

Wiki iliopita , Uganda ilitangazawa kwamba itatuma helikopta za kivita nchini Somalia kukiimarisha kikosi cha wanajeshi 17,000 cha Umoja wa Afrika kilichoko nchini humo kupambana na waasi wa Al-Shabaab wenye mafungamano na Al-Qaeda.

Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wamepelekwa Somalia
Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wamepelekwa SomaliaPicha: picture-alliance/dpa

Akiwa ziarani nchini Uganda juma lililopita sehemu ya ziara yake ya siku 11 barani Afrika, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton, aliipongeza nchi hiyo kwa mchango wake katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Mbali na Uganda nchi nyengine zinazoshiriki katika kikosi hicho ni Burundi, huku Kenya na Djibuti zikisemekana pia kujiunga. Kenya iliingia vitani dhidi ya waasi wa Al-Shabaab ndani ya Somalia mwaka jana baada ya mashambulizi kadhaa ya kiagaidi nchini Kenya ambapo inaaminiwa yalifanywa na waasi hao.

Kikosi cha Umoja wa Afrika kinapanga masahambulizi makubwa katika mji wa kusini wa Kismayu, ambao ni ngome kuu ya Al-Shabaab, kabla ya Agosti 20. tarehe hiyo ndipo muda wa serikali ya sasa ya mpito utakapomalizika rasmi. Tayari bunge limepitisha katiba mpya ya muda na hatua hiyo itafuatwa na uchaguzi wa rais pamoja na kuundwa serikali mpya, itakayochukua nafasi ya utawala utakaoamalizika muda wake.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman, rtr

Mhariri: Josephat Charo.