1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Helen Joseph: alijitolea kupinga ubaguzi wa rangi

Yusra Buwayhid
5 Januari 2021

Helen Joseph mzaliwa wa Uingereza alikuwa na kila sababu ya kuishi maisha mazuri Afrika Kusini, lakini alihatarisha maisha yake kuupinga utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

https://p.dw.com/p/3nWSh

Helen Joseph: mwanaharakati aliyejitolea kupinga ubaguzi

Helen Joseph alizaliwa Uingereza mnamo Aprili 8, 1905, katika kijiji kimoja huko West Sussex. Lakini baadae aliishi miaka mingi jijini London. Alihitimu kama mwalimu wa somo la lugha ya Kiingereza na kwenda India kusomesha na baade kuishia Afrika Kusini katika miaka ya 1930. Huko aliolewa na daktari wa meno na kuwa mmoja wa Wazungu wenye tabaka la juu nchini Afrika Kusini.

Mnamo mwaka 1952, alifunguka macho na kutanabahi kuwa watu wasio weupe wananyimwa haki zao nyingi za msingi, na kujiunga na vuguvugu la kukomesha utawala wa kigaguzi nchini humo akiungana na watu mashuhuri kama vile Winnie Madikizela-Mandela. DW imezungumza na Carl Niehaus, mwanachama mkongwe wa chama cha African National Congress na msemaji wa zamani wa Nelson Mandela, kutaka kujua zaidi kuhusu maisha ya Helen Joseph. 

DW: Ulikutana lini na Helen Joseph?

Carl Niehaus: Nilikutana na Helen Joseph nikiwa na miaka 19 na akawa mmoja wa washauri wa kisiasa wenye ushawishi mkubwa katika maisha yangu.

Helen Joseph alikuwa ni mtu wa aina gani?

Alikuwa ni mtu mwenye nidhamu ya hali ya juu. Alikuwa akiongozwa na maadili ya dini ya Kikristo ya kwamba binadsamu wote wameumbwa sawa na Mungu. Aliamini kwamba serikali ya utawala wa kibaguzi ya wakati huo lazima ipingwe. Kwahivyo, akajiunga na vuguvugu la Congress of Democrats, ambalo baadae liliungana na muungano wa ANC.

African Roots | Helen Joseph
Asili ya Afrika, Helen Joseph

Muungano wa ANC uliunganisha vyama kutoka makabila yote yaliyotenganishwa na serikali ya ubaguzi wa rangi. Kwa nini muungano huo ulimpa nafasi ya uongozi?

Uwezo wake wa kujieleza ulimfanya aonekane kama miongoni mwa viongozi mashuhuri kwenye muungano huo. Alipewa nafasi ya kuwasilisha sehemu ya hati ya Uhuru katika Mkutano wa Watu huko Kliptown na kuongoza maandamano maarufu ya wanawake kwenye majengo ya Union mnamo 1956.

Mnamo Agosti 9, 1956, wanawake 20,000 walieleza hasira zao kuhusu sera za ubaguzi wa rangi, moja ikiwa ni wanawake kulazimika kubeba pasi, hatua ambayo ilipunguza uhuru wao wa kutembea na nafasi za kufanya kazi na kutunza familia zao. Pamoja na mwanamke mweusi, mwanamke wa "rangi" aliyechanganya damu, na mwanamke Mhindi, Helen Joseph aliongoza maandamano hayo na kuacha marundi ya maombi kwenye ofisi ya Waziri Mkuu J. G. Strijdom. Je! Alikuwa na misimamo gani kuhusu haki za wanawake?

Aliamini wanawake wanapaswa kusimama na kupigania haki zao wenyewe. Aliamini  kuwa wanaowanyanyasa wanawake wanastahili kuadhibiwa.

African Roots | Helen Joseph
Helen Joseph, Asili ya Afrika

Vipi mwanamke wa Kizungu mzaliwa wa Uingereza aliweza kujichanganya na upinzani dhidi ya ubaguzi wa rangi?

Alijitolea kupigania jamii isiyo na ubaguzi wa rangi na kupatikana haki sawa kwa wananchi wote wa Afrika Kusini. Alikuwa ni mtu asiye na tabia ya ubaguzi niliewahi kukutana nae maishani mwangu.

Akiwa katika miaka arobaini wakati mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipoanza kuwa na nguvu, Helen Joseph alikuwa miongoni mwa kizazi cha kwanza cha wanaharakati wanaopinga ubaguzi wa rangi. Unamkumbuka zaidi kwa kipi?

African Roots | Helen Joseph
Helen Joseph, Asili ya Afrika

Nilikutana nae wakati akiwa katika miaka ya 70. Alikuwa bado na nguvu zake na akishiriki vilivyo katika mikutno ya harakati za kupinga upaguzi wa rangi. Na huu ndiyo wakati alipohukumiwa kifungo cha nyumbani, huko Northcliff, Johannesburg, kwa takriban miaka mitano.

Mfumo huo wa utawala ulijulikana kwa jinsi ulivyokuwa ukiwaadhibu watu weupe wenzao wanaoshiriki harakati za kupinga ubaguzi. Umewahi kushuhudia matukio yoyote ya ukatili aliyokabiliana nayo Helen Joseph?

Kulikuwa na matokeo mengi ambapo maafisa wa serikali ya ubaguzi wa rangi walikuja nyumbani kwake na kumfatulia risasi licha ya kwamba alikuwa tayari ni mzee asiye na nguvu. Nakumbuka asubuhi moja baada ya tukio kama hilo, nilifika nyumbani kwake na kumkuta akifagia vigae vya madirisha vilivyovunjika na kutawanyika baada ya kumfatuliwa risasi. Niliona hasira machoni mwake. Alikuwa amekasirika sana. Na alisema hivi:Wanaweza kutuua sisi, lakini kamwe hawawezi kuua mapambano ya kutafuta uhuru katika nchi hii.

Nakumbuka pia aliponitembelea nilipokamatwa. Alikuja kwenye kesi yangu pia na akakaa mstari wa mbele kwenye kiti cha magurudumu.

Nikiwa nimekwenda kumtembelea, mara nyingi alinitaka niswali nae mbele ya msalaba wa yesu aliokuwa ameuweka juu ya meza nyumbani kwake.

African Roots | Helen Joseph
Helen Joseph, Asili ya Afrika

Ni wakati gani wa uanaharakati wake ambao bado unaukumbuka hadi leo?

Alihakikisha kuwa wale waliofungwa na familia zao wanakumbukwa. Kila siku ya Krismasi alifanya sherehe saa sita mchana kugonganisha gilasi za mvinyo akisema, "Kwa wenzetu ambao hawapo nasi."

Kipi unachokikumbuka wakati wa siku za mwisho za maisha ya Helen Joseph?

Alikuwa mpiganaji hadi pumzi yake ya mwisho. Nilikuwa kando ya kitanda chake alipokufa siku ya Krismasi saa sita kamili mchana. Alikufa katika hospitali huko Johannesburg iliyopewa jina lake na kuitwa Helen Joseph.

African Roots | Helen Joseph
Helen Joseph, Asili ya Afrika

Je, Helen Joseph wakati wote alikubaliana na viongozi wengine wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi?

Katika mazungumzo yangu ya mwisho na Helen Joseph alinielezea kuwa anahisi Rais Nelson Mandela na chama cha African National Congress walikuwa wanaanza kufanya maelewano mengi wakati wa mazungumzo. Alihisi kuwa mchakato wa upatanishi ulikuwa hauzingatii sana haki.

Carl Niehaus ni mwanaharakati mkongwe wa chama tawala cha African National Congress (ANC), kwa miaka 42 iliyopita. Hivi sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Kitaifa ya Chama cha Maveterani wa Jeshi la Umkhonto Wesizwe.

Mahojiano haya yalifanywa na Thuso Khumalo.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.