Hekaheka za Champions League zarejea tena
7 Desemba 2015Timu tatu kutoka katika Premier League, Manchester United, Chelsea na Arsenal zinaingia uwanjani katikla michezo hiyo ya mwisho zikiwania kubaki katika Champions League wakati awamu ya makundi inafikia mwisho kesho Jumanne na Jumatano.
Nafasi saba katika awamu ya mtoano bado hazina mwenyewe, na mabingwa wanne wa zamani wa Champions League Manchester United, Chelsea, Porto na PSV Eindhoven , ni miongoni mwa timu nyingine saba zenye matumaini ya kupata nafasi katika timu 32 zilizosalia katika ligi hiyo ya Ulaya.
United , Chelsea, Porto na PSV zinajiunga pamoja na VFL Wolfsburg, Roma, Bayer Leverkusen, BATE Borisov, Olympiakos , Arsenal, Dynamo Kiev, Gent ya Ubelgiji, na Valencia zikiwania kusonga mbele.
Timu ambazo tayari zina tikiti zao mkononi katika awamu hiyo ni pamoja na mabingwa watetezi Barcelona, Real Madrid, Paris Saint-Germain, Atletico Madrid,Benfica, Juventus , Manchester City, Bayern Munich na Zenit St Petersburg.
Miongoni mwa mapambano muhimu kesho Jumanne ni pamoja na Wolfsburg ikipambana na kikosi cha kocha Luis Van Gaal cha Man United katika kundi B, wakati PSV Eindhoven inaikaribisha CSKA Moscow. Wolfsburg itaingia katika awamu ya makundi iwapo itapata sare tu, lakini itachukua nafasi ya kwanza katika kundi hilo iwapo itapata ushindi, wakati United itachukua uongozi wa kundi hilo kwa ushindi.
PSV pia inaweza kusonga mbele iwapo itashinda na inaweza kusonga mbele kwa kupata sare iwapo Man United itashindwa.
Mabingwa wa Italia Juventus wana wania kuepuka kupambana na vigogo wa Ulaya katika timu 16 zitakazobakia katika Champions League kwa kupata nafasi ya uongozi katika kundi D nyumbani kwa Sevilla kesho Jumanne.
Timu hiyo iliyofikia fainali msimu uliopita inaongoza kwa pointi mbili ikiitangulia Manchester City na inahitaji sare tu dhidi ya Sevilla ili kuepuka vigogo kama Barcelona , Real Madrid na Bayern Munich katika awamu ya mtoano.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / ape / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman