Merkel atunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima
31 Mei 2019Rais wa chuo cha Havard Larry Bacow aliemtunukia tuzo hiyo Merkel, amemueleza kansela huyo wa Ujerumani kwa miaka 14, kama mwanasiasa mwenye nguvu barani Ulaya.
Chuo hicho kilimsifu Merkel kwa matamshi yake ya "Tutaweza kulisimamia hili" wakati wa mgogoro wa wakimbizi ulioanza mwaka 2015 nchini Ujerumani, pale Kansela huyo alipopokea idadi kubwa ya wakimbizi, na kukosolewa na baadhi nchini mwake.
Chuo cha Havard kimesema uamuzi wa Merkel wa kuruhusu idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji kuingia nchini Ujerumani umeonyesha nia yake ya kusimamia kile anachofikiri kuwa sahihi hata kama hakiridhishi kila mtu, na kuongeza kwamba kansela huyo alionesha pia ukakamavu kama huo wakati wa mgogoro wa kifedha wa barani Ulaya.
Vunja kuta za ujinga
Baada ya kutunukiwa tuzo hiyo, Merkel alihudhuria hafla ya 368 ya kuhitimu kwa wanafunzi wa chuo hicho cha Havard. Katika hotuba yake, Merkel aliwaonya wanafunzi hao dhidi ya kuchanganyikiwa na kuuona uongo kama ukweli na ukweli kama uongo.
"Vunja kuta za ujinga na mawazo finyu, kwani hakuna kitu kinachohitaji kubaki kama kilivyo, " amesema Merkel. "Chukua hatua ya pamoja kwa maslahi ya ulimwengu wa kimataifa. Endelea kujiuliza: 'Je, ninafanya kitu hiki kwa sababu ni sawa, au kwa sababu tu kinawezekana?' Usisahau kuwa uhuru sio kitu ambacho kinaweza kuchukuliwa kwa urahisi," aliongeza kansela huyo wa Ujerumani.
Akizungumza kwa Kijerumani, Merkel amesema uzoefu wake katika siasa umemfunza kwamba kuheshimu mitazamo, dini na utambulisho wa watu wengine kunasaidia kufikia maamuzi mazuri.
Akitoa hotuba yake hiyo katika hafla ya 363 ya kuhitimu wanafunzi wa Chuo cha Havard, Merkel pia amewaonya kwamba kuta ni kitu ambacho kinaweza kuzuia maendeleo yao.
Merkel hakumtaja Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa hotuba yake hiyo, lakini baadhi ya waliokuwa wakimsikiliza walionekana kuunganisha matamshi yake na tabia pamoja na sera za Trump.
dpa/ap