"Hatuogopi tena": Kiongozi wa upinzani Belarus ahimiza Umoja
23 Agosti 2020Katika mahojiano na shirika la habari la AFP, Tikhanovskaya pia amesema watu wa Belarus wameondoa hofu yao na kuiita hatua ya Lukashenko ya kuongeza usalama katika mipaka kuwa ni juhudi tu za kutaka "kuondoa mtazamo katika matatizo yetu ya ndani".
"Najisikia fahari sana na Wabelarusi hivi sasa kwasababu baada ya miaka 26 ya hofu wako tayari kulinda haki zao," alisema mjini Vilnius , ambako alikimbilia baada ya uchaguzi hapo Agosti 9 ambao anadai kupata ushindi.
"Nawataka kuendelea, sio kuacha, kwasababu ni muhimu sana hivi sasa kuendelea kuwa na umoja katika mapambano kwa ajili ya haki," alisema, akizungumza katika mkesha wa maandamano makubwa yanayotarajiwa nchini Belarus siku ya Jumapili.
Wapinzani wa kiongozi huyo aliyekuwapo madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Ulaya wametayarisha migomo na maandamano makubwa katika taifa hilo la zamani wa Umoja wa Kisovieti katika historia ya hivi karibuni kupinga kuchaguliwa kwake tena na wanadai kuwa ajiuzulu.
Hatuwaogopi
"Wanapaswa kuelewa kuwa sisi sio vuguvugu la maandamano. Sisi ni watu wa Belarus na tuko wengi na hatutakaa kando. Hatuwaogopi tena;" Tikhanovskaya aliliambia shirika la habari la AFP.
Mwalimu huyo wa zamani wa somo la Kiingereza na mwanagenzi katika siasa , mwenye umri wa miaka 37 , Tikhanovskaya alijiunga tu katika jukwaa la kisiasa wiki kadhaa kabla ya uchaguzi baada ya mume wake ambaye huandika taarifa katika blog alipozuiwa kujiandikisha kuwa mgombea wa rais.
Hakutoa maelezo juu ya kwanini aliondoka Belarus baada ya uchaguzi lakini alisema alifanya hivyo kwa ajili ya watoto wake na waungaji wake mkono wanasema alikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa maafisa wa Belarus. Ametoa wito wa uchaguzi mpya na kusema hana mpango wa kugombea katika uchaguzi wowote hapo baadaye.
Tikhanovskaya pia ameteua baraza la uratibu ambalo anataka kujadili "makabidhiano ya amani ya madaraka" lakini chombo hicho cha upinzani kinachunguzwa nchini Belarus kuwa ni jaribio lisilo halali kisheria kumuondoa madarakani rais Lukashenko.
Alipoulizwa kitu ambacho kinaweza kumsukuma Lukashenko kufanya majadiliano na upinzani , alisema: "Nafikiri hana chaguo." Lakini alisema kwamba majadiliano yanapaswa kuanza haraka iwezekanavyo "ili kutoruhusu mzozo huu kuwa mkubwa zaidi".