Hatua za kuwarejesha makwao waliokataliwa kinga ya ukimbizi
23 Februari 2017Tunaanza na mpango wa serikali kuu kuwarejesha haraka haraka wahamiaji ambao hawana nafasi ya kukubaliwa kinga ya ukimbizi. Kuna wanaoukosoa mpango huo. Gazeti la "Südwest Presse" linaandika: "Serikali kuu ya Ujerumani imejiwekea lengo maalum kwa mwaka huu wa 2017; inataka idadi kubwa zaidi ya wahamiaji warejeshwe makwao kuliko miaka iliyopita. Mpango huo wa kulazimishwa watu kurejea makwao, ingawa unaonekana kuwa ni wa kuchukiza, lakini ni wa lazima watu wakitilia maanani upande wa pili wa kinga ya ukimbizi. Mpango wa kurejeshwa makwao waafghanistan unakosolewa mno na kwa sababu zinazoeleweka. Kwa wengi wanaorejeshwa huko, maisha yao hayako salama. Asiyekuwa na familia ya kumpokea, hana nafasi yoyote ya kufanikiwa. Ndio maana idara husika za Ujerumani zinabidi ziwe macho ipasavyo na kuchunguza kwa kina, kila kadhia husika.
Mivutano ya kisiasa imechelewesha uamuzi
Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linahisi serikali kuu imehitaji muda mrefu kupitisha uamuzi huo. Gazeti linaendelea kuandika: "Kidogo kidogo na licha ya malalamiko, serikali kuu inajaribu kuidhibiti hali ya mambo. Kwa muda mrefu walizozana na kutofautiana kuhusu sera za mapokezi kwa namna ambayo walishindwa kubuni mwongozo bayana wa uchunguzi na hatua kali dhidi ya wale wanaoishi kinyume na sheria au wanaovunja sheria nchini Ujerumani.
Palihitajika kwanza kuitokea shambulio la kigaidi la Berlin lililoangamiza maisha ili serikali ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na SPD kuzindukana:Mbali na mapokezi ya ukarimu kwa wengi wanaoandamwa, wanaonyanyaswa na wahanga wa vita, inabidi pia zichukuliwe hatua kali dhidi ya wale wanaotumia vibaya ukarimu wa wajerumani, naiwe kwa malengo ya kidini, kihalifu au kigaidi."
Nyota ya Martin Schulz yaking'aria chama cha SPD
Tangu spika wa zamani wa bunge la Ulaya Martin Schulz achaguliwe kugombea kiti cha kansela kwa tikiti ya chama chake cha Social Democrat-SPD, haiba ya chama hicho imeanza upya kung'ara. Uchunguzi wa maoni ya wananchi unakiweka takriban mstari mmoja na vyama ndugu vya CDU/CSU. Gazeti la " Rhein-Neckar-Zeitung" linaandika: "Tafiti za maoni ya umma daima huzusha maajabu.Na baadhi ya wakati kinachoashiriwa msimu wa machupuko,kinatoweka msimu wa kiangazi unapowadia. Lakini maajabu yanayosababishwa na Martin Schulz yaliyopelekea chama cha SPD kuzidi umaarufu wake kupita kiasi, ni ya aina nyengine, na hayaonyeshi dalili ya kufifia-kinyume kabisa yanaonyesha yataselelea. Na hali hiyo inaweza kusababisha CDU/CSU wakapoteza kiti cha kansela.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Gakuba Daniel