Hatua kali za usalama kufuatia shambulio la kigaidi Tunisia
27 Juni 2015Watalii wamejazana katika uwanja wa ndege wa Hammamet karibu na mji wa mwambao wa Sousse ambapo kijana mmoja aliwauwa kwa bunduki ya rashasha aliokuwa ameificha kwenye mwamvuli wake wa pwani watu 39 wengi wao wakiwa watalii hapo Ijumaa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tunis mapema Jumamosi (27.06.2015) Habib Essid amesema "mapambano dhidi ya ugaidi ni wajibu wa taifa" . Amesema wako kwenye vita dhidi ya ugaidi ambao unatowa tishio kubwa kwa umoja wa kitaifa katika kipindi hiki kigumu inachopitia taifa.
Ametangaza hatua kadhaa kali kupambana na itikadi kali ikiwa ni pamoja na kuchunguza michango inayogharamia mashirika yanayoshukiwa kuendeleza itikadi kali, kufunga misikiti themanini ambayo haiko chini ya udhibiti wa serikali na kuyatangaza maeneo fulani ya milimani kuwa maeneo ya kijeshi.
Dola la Kiislamu ladai kuhusika
Kijana wa kiume aliyehusika na shambulio hilo ametambuliwa kuwa ni Seifeddine Rezqui mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kairouan.Kundi la Dola la Kiislamu kupitia mtandao wa Twitter limedai kuhusika na shambulio hilo.
Katika hoteli ya Marhaba ambako shambulio hilo limefanyika mabasi yamekuwa yakiwaondowa watalii Jumamosi.Wakati hoteli hiyo haikufungwa mashirika yanayoshughulikia watalii yamemtaka kila mtu aondoke kwenye hoteli hiyo.
Mkurugenzi wa hoteli hiyo Mohammed Becheur amesema yumkini wakawa hivi sasa hawana wateja kabisa lakini wataendelea kushikilia wafanyakazi wao na kuongeza kwamba hoteli hiyo ya vyumba 370 imekuwa ikikaliwa kwa asilimia 75 kabla ya shambulio hilo.
Athari kwa utalii
Utalii unachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tunisia na tayari umeshuka kwa asilimia 25 kufuatia shambulio la kigaidi kwenye makumbusho ya taifa lililouwa watu 22 katika mji mkuu wa Tunis hapo mwezi wa Machi.
Kampuni za safari za Uingereza Thomson na First Choice zimesema zimekuwa zikiwarudisha nyumbani maelfu ya watalii kutoka Tunisia na zinafuta safari zote za ndege kwenda nchini humo wiki ijayo.
Safari za watalii kutoka Ireland kwenda Tunisia zimeendelea kufuatia shambulio hilo lakini mawakala wa safari wanawarejeshea fedha zao zote wale wanaofuta safari zao. Slovakia imepeleka ndege kuwachukuwa raia wake 150 ambao hivi sasa wako Tunisia. Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje na mashirika ya watalii ya nchi za Scandinavia wamesitisha safari zote za ndege kwenda katika nchi hiyo ya Afrika kaskazini kwa msimu wote uliobakia.
Wizara ya Afya ya Tunisia imethibitisha uraia wa watu kumi kati ya wahanga 39 wa shambulio hilo wakiwemo Waingereza wanane,Mbelgiji mmoja na Mjerumani mmoja. Serikali ya Ireland imesema muuguzi mmoja wa nchi hiyo pia ni miongoni kwa watu waliouwawa.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP
Mhariri : Yusra Buwayhid