1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua kali za ulinzi mkesha wa mwaka mpya magazetini

Oumilkheir Hamidou
3 Januari 2017

Mjadala uliohanikiza kufuatia hatua kali za usalama katika mkesha wa mwaka mpya katika jiji la Cologne na kwengineko nchini Ujerumani na shambulio la kigaidi mjini Istanbul ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2VBnD
Deutschland Köln Silvesternacht - Personenkontrollen am HBF
Picha: picture-alliance/dpa/H. Kaiser

 

Tunaanza lakini na mjadala uliopamba moto humu nchini baada ya mwenyekiti wa chama cha walinzi wa mazingira die Grüne, Simone Peter kuwatuhumu polisi "kufanya ubaguzi" walipowalenga zaidi vijana wanaotokea Afrika kaskazini katika hatua za ulinzi mnamo mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne. Matamshi yake yamekosolewa  tangu na wahariri wa magazeti mpaka na viongozi wenzake chamani. Gazeti la Donaukurier linaandika:"Mkesha wa mwaka mpya ulikuwa tulivu kwa sehemu kubwa kwasababu uwanja mkuu mbele ya kanisa kuu la Dom mjini Cologne ulikuwa sawa na "jela."Tuhuma za "kubaguliwa watu kwasababu ya sura zao," zilizotolewa na mwanasiasa wa chama cha waalinzi wa mazingira die Grüne, Simone Peter, ni upuuzi mtupu. Vikosi vya usalama vimewalenga wale ambao mwaka mmoja uliopita walihusika na mamia ya visa vya uhalifu.Yadhihirika kana kwamba Simone Peter ameshasahau yaliyotokea."

Polisi wastahiki sifa na sio lawama

Gazeti la Flensburger Tageblatt linahisi, badala ya kukoselewa, polisi wanastahili kusifiwa. Gazeti linaendelea kuandika: "Ni jukumu la polisi kuingilia kati usalama wa jamii  unapatishiwa au unapoingia hatarini. Na hivyo  ndivyo walivyofanya. Na walichokifanya ni kile kile ambacho wananchi walikuwa wakikitegemea-yaani kuwajibika ipasavyo ili kuhakikisha usalama. Kwa hivyo polisi wanastahiki kimoja tu, shukurani na sio kutiwa lawamani. Cha kutisha hasa ni ile hali kwamba licha ya  hatua kali za vikosi vya usalama, vijana wa kutoka Afrika kaskazini kwa mara nyengine tena wameagana na kujitokeza kwa wingi na kwa shari. Sheria na nidhamu, vijana hao wanaoomba kinga ya ukimbizi, wanaonyesha hawazijali. Suala mtu analobidi kujizuliza: Nini cha kufanya mbele ya vijana kama hao wasioogopa kurudia vitimbi vyao?"

Shambulio la kigaidi Istanbul

Shambulio la kigaidi lililotokea mwaka mpya katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Uturuki-Istanbul nalo pia limegonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani. Gazeti la Mannheimer Morgen linaandika: "Balaa kubwa linaikumba Uturuki. Hakuna nchi yoyote mwanachama wa jumuia ya kuijihami ya NATO inayosumbuliwa mno na ugaidi kama Uturuki. Inahitaji pia mshikamano wa nchi za Ulaya-ingawa Erdogan anataka kuigeuza nchi  yake kuwa nchi isiyofuata sheria. Risala la rambi rambi pekee hazitoshi. Watu wanabidi washirikiane, kwasababu shambulio la Istanbul lingeweza pia kuvilenga vilabu vya usiku au disco, mjini Berlin  au Paris. Wanamgambo wa dola la kiislam IS wanaeneza vita sio tuu katika eneo la mashariki ya kati bali pia katika nchi za magharibi. Lengo lao ni moja tu: kuueneza hofu na wasi wasi; naiwe nyumbani mjini Berlin au likizoni mjini Istanbul."

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga