1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua dhidi ya ugaidi na mikutano ya mwanzoni mwa mwaka ya vyama vya CSU na kile cha FDP

Oumilkher Hamidou7 Januari 2010

Wahariri wanajiuliza wapiga kura wanaiangaliaje serikali mpya ya muungano wa nyeusi na manjano?

https://p.dw.com/p/LNe6
Rais Obama akizungumzia uzembe uliotokea na ambao nusra ungegharimu maisha ya abiria karibu mia tatu wa shirika la ndege la Delta huko DetroitPicha: AP

Uzembe wa idara za upelelezi nchini Marekani na mikutano ya jadi ya mwanzoni mwa mwaka ya vyama vidogo viwili shirika katika serikali kuu ya muungano mjini Berlin,FDP mjini Stuttgart, na CSU mjini Kreuth, ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini hii leo.

Tuanzie lakini Marekani ambako gazeti la "SAARBRÜCKER ZEITUNG" linaandika kuhusu njama ya kutaka kuiripua ndege ya abiria ya Marekani-Delta- ilipotaka kutuwa huko Detroit.Ggazeti linaandika:

Salama msafiri mmoja alikuwa macho na jasiri kuweza kuepusha balaa la kushambuliwa ndege ya Delta mjini Detroit. Lakini Marekani isitegemee bahati kama hiyo kutokea tena. Na hayo rais Barack Obama anayajua vilivyo, na ndio maana amezikosoa vikali idara za upelelezi. Kinyume na hali namna ilivyokua baada ya September 11,safari hii ikulu ya Marekani, inayoongozwa na Barack Obama,haijaficha sehemu ya makosa yaliyofanywa na serikali yake katika balaa ambalo lilikua nusra litokee. Hali ya uwazi ni hatua ya mwanzo tuu,nyengine zinabidi haraka zifuate.Miongoni mwa hatua zinazohitajika haraka ni pamoja na kuziorodhesha pamoja data zote zilizoko kuhusu watuhumiwa na wengineo.Jengine ambalo pia ni muhimu ni kufafanua kikamilifu jukumu la kila mmoja miongoni mwa wakuu wa idara za upelelezi nchini humo.

Gazeti la "DRESDNER NEUESTE NACHRICHTEN linahisi kisa cha Disemba 25 kitamfanya rais Barack Obama abadilishe mkondo wa siasa aliyokua akiifuata hadi sasa.Gazeti linaendelea kuandika:

Haisaidii kitu chochote kukusanya kwa pupa data zote zilizoko,na kushindwa kutambua baadae ipi iko wapi. Na maadhara ni makubwa hasa pale afisa wa Marekani anapoonekana kusahau aliyoambiwa,pale bwana mmoja mashuhuri nchini Nigeria alipoonya mwanawe wa kiume anafuata itikadi kali ya kidini.Uzembe katika mfumo wa usalama ni sawa na kumwagia mafuta ya moto katika kidonda cha Marekani. Kwa hivyo, lawama kali zilizotolewa na rais wa Marekani Barack Obama hazikua za bure. Mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel ambae angependelea zaidi kushughulikia mageuzi ya mfumo wa afya na kutawala kwa moyo wa mdahalo na maridhiano,analazimika kukabiliana na vita dhidi ya magaidi. Hali hiyo itamlazimisha pia abadilishe mkondo wa siasa yake.

Deutschland Heilige Drei Könige FDP in Stuttgart
Waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle (kati)akishangiriwa baada ya hotuba yake mjini StuttgartPicha: AP

Mada yetu ya mwisho inahusu mikutano miwili inayoitishwa kawaida kila mwanzoni wa mwaka mpya na vyama viwili vidogo vya kisiasa humu nchini-CSU na FDP. Mwaka huu chama kidogo cha kiliberali cha FDP ni mshirika katika serikali kuu ya muungano mjini Berlin pamoja na vyama ndugu vya CDU/CSU.Na chama hicho hasa ndicho kilichohanikiza wakati wa mkutano wake katika mji wa kusini wa Stuttgart.Gazeti la "MÜNCHNER MERKUR" la mjini Münich linaandika:

Hakuna majibu yoyote sahihi yaliyotolewa kuhusu namna ya kusawazisha nakisi iliyokithiri ya bajeti, na namna ya kuleta uwiano kati ya matakwa ya kupunguza kodi ya mapato na umuhimu wa kufunga mikaja.Miito ya kupunguza kodi na kuanzisha mageuzi ya kisiasa ya kiroho,imetosha kuwaridhisha wafuasi wa FDP waliohudhuria mkutano huo mjini Stuttgart.Kwa jinsi gani lakini raia wanaiunga mkono serikali ya muungano wa nyeusi na manjano,,jibu litapatikana baada ya uchaguzi katika jimbo la North Rhine Westphalia mwezi May ujao.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou /Inlandspresse

Mhariri: Miraji Othman