Hatma ya serikali ya pamoja nchini Zimbabwe, kujulikana leo.
19 Januari 2009Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Kiongozi wa Chama cha Upinzani nchini humo Morgan Tsvangirai, wanakutana leo na viongozi wa Jumuia ya Maendeleo kusini mwa Afrika -SADC- kujaribu kuokoa makubaliano ya kuundwa kwa serikali ya pamoja nchini humo, yaliyolega mara tu baada ya kusainiwa, mwezi Septemba mwaka jana.
Rais wa Afrika kusini Kgalema Motlanthe, pamoja na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, ambaye pia ni msuluhishi mkuu wa mzozo huo wa kisiasa, Thabo Mbeki na Rais Armando Guebuza wa msumbiji tayari wamewasili nchini humo kwa ajili ya kukutana na viongozi wa pande zote zinazopingana, kujaribu kuokoa makubaliano hayo.
Katibu Mtendaji wa SADC, Tomaz Salamao aliwasili jana nchini humo kwa ajili ya maandalizi ya mikutano huo.
Jana, Rais Mugabe, alitishia kuvunja mazungumzo hayo ya kugawana madaraka, iwapo upinzani watakataa mpango huo kwa kusisitiza kuwa, aidha wakubali ama makubaliano hayo yavunjwe.
Nacho Chama cha Upinzani nchini humo kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai, cha Movement for Democratic Change -MDC- kimesisitiza kuwa hakitashiriki katika serikali hiyo ya pamoja, mpaka pale masharti yao yote, yatakapokubaliwa, ikiwemo haki sawa katika uteuzi wa baraza la mawaziri, ambapo pia wamejumuisha malalamiko yao kwamba wafuasi wao walitekwa na kuteswa na taasisi za usalama, za serikali.
Chama hicho cha MDC, kimetoa wito wa kumalizwa kwa mjadala huo, hata kama watafanikiwa au kushindwa matakwa yao kutokana na kudai kuwa, Wazimbabwe hawawezi kuendelea kuwa katika mpango huo usiokwisha.
Rais Robert Mugabe wa Ziimbabwe na Kiongozi wa Upinzani Morgan Tsvangirai mpaka sasa bado hawajakubaliana jinsi ya kugawana madaraka katika nafasi za mawaziri, licha ya kuingiliwa kati mara kadhaa na viongozi wa nchi za Afrika.
Mswada wa marekebisho kuhusu makubaliano hayo ya kugawana madaraka utawasilishwa katika bunge la nchi hiyo litakapoanza vikao vyake siku ya Jumanne.
Kutoafikiana kwa viongozi hao kumesababisha madhara makubwa kwa raia wa kawaida nchini humo, ambapo nusu yao wanaishi kwa kutegemea chakula cha misaada, kupanda kwa gharama ya maisha kwa kiwango kikubwa na ugonjwa wa klipindupindu ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 2 nchini humo.
Kiongozi wa upinzani nchini humo, Morgan Tsavangirai aliwasili siku ya Jumamosi nchini humo, ikiwa ni mara ya kwanza toka mwezi Novemba mwaka jana, ambapo muda wake mwingi ameutumia akiwa nchini Botswana.
Mara tu baada ya kuwasili nchini humo, aliwaambia waandishi wa Habari kwamba anamatumaini kuwa mkutano wa leo, utatoa suluhisho la mwisho, na kuonya kuwa chama chake cha MDC hakitapeleKeshwa kwenye makubaliano; ambayo hayatakidhi matakwa ya watu wa nchi hiyo.