1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya kesi ya Kenyatta yajadiliwa ICC

8 Oktoba 2014

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anahudhuria kikao hicho akiwa kama raia wa kawaida baada ya kuchukua uamuzi wa khiari wa kuyakabidhi madaraka kwa makamu wake William Ruto hapo jana(07.10.14)

https://p.dw.com/p/1DRzY
Kikao cha hoja ya kesi ya Kenyatta,ICC
Kikao cha hoja ya kesi ya Kenyatta,ICCPicha: ICC

Nje ya mahakama hiyo ya Icc Uhuru Kenyatta alilakiwa asubuhi leo 08.10.2014) na kikundi kidogo cha raia wa Kenya walioandamana huku wakicheza na kuimba pamoja na kubeba mabango yaliyoandikwa meneno ya kuitaka mahakama ya Icc Kumuachilia rais wao. Ndani ya jengo la mahakama Kikao hicho maalum kinaongozwa na jopo la majaji watatu Jaji Oniko Ozaki kutoka Japan amekifungua kwa kusoma kile kinachotarajiwa hadi kufikia mwisho wa siku hii muhimu kabisa katika kesi dhidi ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. Jaji akisoma maelezo hayo Bwana Kenyatta alikuwa anatazama kwa makini huku akionekana shujaa na asiyekuwa na uwoga wowote.

Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake William RutoPicha: picture alliance/dpa

Kenyatta akiwa amevalia suti ya rangi ya mkaa na tai ya rangi ya kibuluu alionekana akiwa mtulivu wakati huo na hata baada ya kutakiwa na jaji Oniko Ozaki kujibu ikiwa ameleewa kilichokuwa kimeelezwa,alikaa kimya bila ya kutikisika na badala yake wake alisimama na kutoa malezo kwamba Kenyatta hatosema chochote katika kikao cha leo na kwamba yeye kama wakili ndiye atakayechukua jukumu hilo.

Jaji Oniko Ozaki amesema kwakuwa Kenyatta yuko The Hague akiwa mtu mwenye hadhi mbili yaani,raia wa Kawaida lakini vile vile ni rais wa Jamhuri ya Kenya kuna masuala mengi ambayo atalazimika kuyajibu kama raia wa kawaida na sio kama kiongozi wa nchi. Upande wa Mashtaka uliopewa nafasi ya mwanzo hii leo kutoa hoja zake juu ya kesi hii umesema hauamini itakuwa jambo la busara mahakama kuchukua uamuzi wa kuweka tarehe maalum ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kwakuwa ni wazi serikali ya Kenya imekuwa ikikataa kushirikiana na mahakama hiyo katika kutoa nyaraka muhimu na hasa zile za benki za bwana Kenyatta.Upande huo wa mashtaka umeitaka mahakama kuiakhirisha kwa muda usijulikana kesi hiyo.

Hata hivyo upande wa utetezi ambao pia umepewa nafasi kuzungumzia juu ya hoja hiyo ya kurefushwa muda wa kesi hiyo kwa kipindi kisichojulikana,umeonekana kutokubaliana na hilo ukitoa hoja kwamba mashahidi wa upande wa mashtaka wameshakiri kusema uwongo katika kesi hiyo na wengine wamejitoa.Wakili wa Uhuru Kenyatta Stephen Kay amesema hakuna ushahidi unaonyesha kwamba mteja wake amezuia juhudi za kupatikana ushahidi kama inavyodaiwa na upande wa mashtaka.

Ikumbukwe kwamba mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo Fatoue Bensouda ambaye pia anahudhuria kikao hiki ameshatoa madai kwamba wanashindwa kupata ushahidi kwakuwa mashahidi wamekuwa wakipewa vitisho sambamba na serikali ya kenya kukataa kutoa ushirikiano muhimu.Hadi wakati huu kiasi mashahidi saba wa upande wa mashtaka wamejiondoa katika kesi hiyo kukiweko madai kwamba walichukua hatua hiyo baada ya kupewa hongo pamoja na vitisho.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou BensoudaPicha: AP

Majaji huenda wakaamua kuridhia kesi iendelee au kuifutilia mbali baada ya upande wa mashakata kukiri kwamba hawana ushahidi wa kutosha ingawa uamuzi huo wa majaji hautarajiwa hii leo.Ikumbukwe kwamba Bwana Kenyatta mwenye umri wa miaka 52 anakabiliwa na mashtaka matano kuhusiana na dhima yake katika ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 zilizosababisha mauaji ya kiasi watu 1200 na wengine laki 6 wakaachwa bila makaazi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman