1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatma ya Gbagbo yaanza kujadiliwa Icc

19 Februari 2013

Waendesha Mashtaka kwa mara ya kwanza wanaieleza mahakama juu ya ushahidi wao unaomtuhumu Gbagbo kuhusika moja kwa moja na uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini mwake.

https://p.dw.com/p/17hHh
Laurent Gbagbo akiwa ICC Desember 2011
Laurent Gbagbo akiwa ICC Desember 2011Picha: dapd

Mamia ya wafuasi wa aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo wameandamana nje ya mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu mjini The Hague, wakati mahakama hiyo ikianza kikao chake cha kwanza kusikiliza ushahidi wa waendesha mashtaka utakaoamua ikiwa Gbagbo ana kesi ya kujibu au la.

Kinachojadiliwa

Kikao hicho cha kwanza kabisa kinachosikiliza hoja za upande wa waendesha mashtaka juu ya tuhuma za kumuhusisha na uhalifu Laurent Gbagbo kimefunguliwa hivi punde huku Gbagbo mwenyewe aliyeonekana kuwa mtulivu akiwepo mahakamani. Kikao hicho ambacho kimsingi kitahitajika kutoa maamuzi ya ikiwa Gbagbo ana kesi ya kujibu au la katika kesi ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu inayomkabili kimefunguliwa na Jaji Silvia Fernandez de Gurmendi.

Ghasia zilipozuka Abidjan
Ghasia zilipozuka AbidjanPicha: AP

Wakati akiingia katika ukumbi huo wa mahakama Laurent Gbagbo aliwaamkia waandishi wa habari pamoja na wafuasi wake waliofika katika mahakama hiyo. Muda mchache kabla ya kuanza kikao hicho waandamanaji wanaokadiriwa kufikia hadi 300 walishiriki katika maandamano ya amani kupinga hatua ya kuwekwa kizuizini Laurent Gbagbo aliyeshindwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 na mpinzani wake rais wa sasa wa Cote d'Ivoire, Alassane Outtara.

Wafuasi wa Gbagbo wajitokeza

Miongoni mwa waandamanaji hao alikuweko pia Hubert Seka mwenye umri wa miaka 43 aliyesafiri hadi The Hague akitokea Italia, aliyesikika akisema na hapa tunanukuu

''Tuko hapa kwa sababu leo rais Gbagbo anafikishwa ICC pamoja na kwamba ni rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na tuhuma dhidi yake zinapaswa kumkabili Allasane Outtara.''

Gbagbo mwenye umri wa miaka 67 ni kiongozi wa kwanza wa nchi kufikishwa mbele ya mahakama hiyo ambako majaji wanajiandaa kutoa kauli yao kuthibitisha tuhuma zinazomkabili za kupanga kampeini ya ghasia za mwaka 2010 hadi 2011kufuatia kipindi cha mvutano baada ya uchaguzi, ghasia zilizosababisha vifo vya watu 3,000 nchini humo.

Wengi wa watu walioandamana hii leo mjini The Hague walisafiri kutokea sehemu mbali mbali za Ulaya wakiwa wamevalia kofia na nywele bandia zilizopakwa rangi za kitaifa huku wakipeperusha bendera ya Cote d'Ivoire huku wakisikiliza muziki na hotuba kadhaa.

Rais Alassane Ouattara
Rais Alassane OuattaraPicha: Reuters

Kimsingi kikao cha leo kitawasikiliza waendesha mashitaka watakaotoa ushahidi wao wanaosema unadhihirisha kwamba kiongozi huyo wa zamani wa Cote d'Ivoire ana kesi ya kujibu kwa kuhusika na uhalifu ikiwemo kuua, ubakaji na utesaji katika ghasia zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa rais uliozusha utata mwaka 2010. Gbagbo hata hivyo anashikilia kwamba hana hatia. Zoezi hilo la kusikiliza ushahidi litaendelea hadi Februari 28 ambapo waendesha mashitaka watajieleza na majaji watalazimika kutoa uamuzi ikiwa ushahidi huo unatosha kuanzisha kesi kamili dhidi ya Gbagbo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo