Hatima ya Nato na amani ya Mashariki ya Kati Magazetini
16 Februari 2017Tunaanza na hatima ya jumuia ya kujihami ya NATO. Gazeti la "Der neue Tag" linaandika: "Watu hawapaswi kushangaa kwamba serikali mpya ya Marekani, kinyume na zilizotangulia, haitomalizikia kwa kuwaonya tu washirika wake wa Ulaya. Na sio tu kwa sababu ya vitisho alivyotoa Rais Donald Trump katika kampeni zake za uchaguzi, bali kwa sababu subira ya wamerekani kwa wazungu wa Ulaya, na kinyume chake, inafikia kikomo. Juhudi za kudhamini ulinzi wao wenyewe ni kwa masilahi ya nchi za Ulaya na hilo limeingia midomoni tangu muda mrefu uliopita. Ndio maana macho ya washirika yanakodolewa Ujerumani. Lakini jeshi la shirikisho Bundeswehr hali yake hairidhishi."
Bajeti ya ulinzi izidishwe
Marekani inawataka washirika wa jumuia ya kujihami ya NATO wawajibike kikamilifu katika kuhakikisha usalama ulimwenguni. Lakini wito huo si wa leo, linaandika gazeti la "Wiesbadener Kurier: "Kwamba nchi za Ulaya zilitakiwa ziongeze bajeti ya ulinzi kwa asilimia mbili ya pato la ndani kwa kila nchi, uamuzi huo sio wa leo. Tangu ulipopitishwa, muda mrefu umepita. Ujerumani ndio kwanza imefikia asilimia 60 ya lengo hilo. Kinachowashughulisha wamarekani sio pekee hesabu, wanataka pia ziungwe mkono harakati za kijeshi na hasa Mashariki ya Kati."
Hatima ya juhudi za amani mashariki ya kati
Mada yetu ya pili magazetini inahusu hatima ya utaratibu wa amani ya Mashariki ya Kati kwa kuzingatia mazungumzo aliyokuwa nayo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani Donald Trump. Gazeti la "Rhein-Zeitung" la mjini Koblenz linaandika: "Wakijivunia uungaji mkono wa Donald Trump, waisrael hawajali chochote, wanaendelea na sera yao ya ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi. Wiki iliyopita, bunge la Israel limepitisha sheria inayohalalisha nyumba 4000 za walowezi wa kiyahudi zilizojengwa tangu zamani katika ardhi za wapalastina. Ikiwa marafiki wa Israel wanashindwa kuafikiana na kupinga sera ya kueneza makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi, basi mzozo huo unatishia kuzidi makali. Zaidi ya hayo kuna kitisho cha kuripuka mvutano kati ya nchi za kiarabu na ulimwengu wa magharibi. Mataifa ya kiarabu kamwe hayatoachana na lengo la kuundwa dola la Palastina."
Malipo sawa ya uzeeni hadi mwaka 2025
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na malipo ya uzeeni. Waziri wa ajira wa serikali kuu ya Ujerumani, Andrea Nahles wa kutoka chama cha Social Democrat, amesema kiwango cha malipo ya uzeeni kwa wastaafu wa sehemu ya mashariki ya Ujerumani kitakuwa sawa na kile cha wenzao wa magharibi hadi ifikapo mwaka 2025. Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika: "Baada ya vuta nikuvute ya miaka kadhaa, hatimae ratiba imeshaandaliwa, kusawazishwa malipo ya uzeeni ya sehemu ya mashariki na ile ya magharibi mwa Ujerumani. Bashasha na uchezi wa waziri wa ajira Andrea Nahles anaetokea eneo la Mto Rhine zimemshinda nguvu waziri mkakamavu wa fedha kutoka jimbo la Badenwürttemberg, Wolfgang Schäuble. Hata hivyo kiwingu kimetanda katika furaha hiyo, nacho ni jee kazi sawa, malipo sawa. Hiyo inasalia kuwa ndoto.
.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Grace Patricia Kabogo