1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uchumi

Hatari tano kwa biashara Afrika Mashariki 2018

9 Januari 2018

Je ni masuala yepi yanayotarajiwa kutoa mwelekeo wa jinsi ambavyo uwekezaji na biashara zitakavyoendelea katika kanda ya Afrika Mashariki? Shirika la Control Risks limetambua hatari tano kwa biashara Mashariki 2018.

https://p.dw.com/p/2qaQX
East African Community Gipfel Tansania Arusha
Picha: picture-alliance/dpa/Xinhua

Kenya inarudi katika hali ya utulivu kisiasa baada ya uchaguzi wa rais uliochukua muda mrefu na uliokumbwa na misukosuko. Hata hivyo changamoto zitaendelea kuwepo mwaka huu kwa mashirika yanayohudumu nchini humo na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Hayo ni kwa mujibu wa shirika la kitaalamu Control Risks linalochambua hatari na udhibiti wa hatari za kibiashara na uwekezaji.

Daniel Heal ambaye ni mshirika mkuu wa shirika hilo katika kanda ya Afrika Mashariki, amesema "mwaka 2018 ni mwaka wenye matumaini kwa Kenya na Afrika Mashariki.

Tayari tumeanza kuona imani ya wawekezaji ikirejea taratibu kufuatia udhibiti wa kisiasa nchini Kenya na azma katika kuendeleza miradi mipya ya miundo mbinu Kenya na katika kanda hiyo kwa jumla. Tunatarajia hili kuendelea hadi mwisho wa mwaka huu."

Hata hivyo Daniel anasema nchini Kenya, hitaji la kulipa awamu ya kwanza ya mkopo wa fedha za Eurobond ambazo zilikuwa dola milioni 774.8, linapaswa kuishawishi serikali kudhibiti ukopaji na matumizi kabla deni kufikia kiwango cha kutodhibitika.

Kenia Skyline Nairobi
Jiji la Nairobi nchini Kenya.Picha: picture-alliance/World Pictures/Photoshot/P. Phipp

Hatari ya kuchafua sifa

Kenya inayo hamu kubwa ya kukopa, na haijazitambua athari zake kisiasa. Ndivyo anavyosema Daniel. Japo nchi hiyo haijaonesha kuwa itashindwa kuyalipa madeni yake, kuongezeka kwa viwango vya riba na mabenki ya kimataifa kupunguza utayari wao wa kupeana mikopo zaidi, itasababisha upungufu wa matumizi katika sekta ya umma.

Mizozo kuhusu madeni inaibua hatari ya kuharibu jina. Nchi katika eneo hilo zenye uchumi mpana kama Kenya na Ethiopia, zitaepuka mizozo ya madeni. Lakini wawekezaji watakuwa na wasiwasi kuhusu udhibiti wa mikopo kwa muda mrefu. Serikali katika eneo hilo zitahitaji kupiga hatua kubwa katika kudhibiti fedha za umma, zipunguze matumizi na zidhihirishe mikakati ya uwajibishwaji ili kuepuka athari-hasi katika uchumi.

Kuimarishwa kwa miundo mbinu Afrika Mashariki kunatarajiwa kuendelea mwaka 2018. Hata hivyo miradi kati ya mataifa hayo itategemea ushirikiano wa kisiasa ulio imara na wa karibu kati ya serikali za kanda hiyo, hali inayoongeza hatari kisiasa. Kutilia maanani bidhaa za ndani kutaibua hatari kuhusu jina la nchi kwa wawekezaji wa kikanda. Kadhalika masuala ya ardhi na jamii yatahitaji wawekezaji kujitokeza kikamilifu kuyasuluhisha ili kuepuka mikwamo yoyote ya utekelezaji miradi.

Mivutano kati ya serikali kuu ya serikali za kaunti

Uganda Präsident Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: Reuters/J. Akena

Mivutano kati ya serikali kuu ya Kenya na serikali za kaunti nchini humo huenda ikasababisha hatari za kisiasa. Serikali itahitaji kuimarisha udhibiti na ilenge kuimarisha mazingira mazuri ya kushirikiana na serikali za kaunti ili kuepuka hatari za kisiasa. Pia itahitaji kulenga kuichochea sekta binafsi kwa kuangalia upya viwango vya riba na kuwahimiza wawekezaji binafsi zaidi kushiriki katika miradi ya miundo mbinu. Aidha itahitaji kupunguza vizingiti vya kiserikali.

Hali isiyotabirika ya utungaji sera nchini Tanzania, itaendelea kuzusha changamoto kubwa za kiudhibiti kwa wawekezaji wa ndani na kikanda. Udhibiti wa madaraka wa Rais John Magufuli unaendelea kuwa imara, na uongozi wake wa kiimla na utata wa namna anavyochukulia miswada ya sekta ya uchimbaji madini, kama njia ya kuongeza mapato ya serikali na kukabiliana na upungufu, zinazusha hatari kadhaa za muda mfupi na wastani kwa udhibiti na uwekezaji.

Nchini Uganda mazungumzo kuhusu mrithi wa rais Yoweri Museveni yataendelea. Matukio katika chama tawala National Resistance Movement (NRM) huenda yataibua mkanganyiko katika utungaji sera na kusababisha ucheleweshaji unaoweza kuathiri biashara.

Nchini Ethiopia, huenda serikali ikakumbwa na maandamano zaidi ikiwa haitapanua uwanja wa siasa na kufanya baadhi mabadiliko katika uongozi. Hali hii itasababisha hatari kwa biashara katika maeneo ya Amhara na Oromia na katika mpaka kati ya Oromia na serikali ya jimbo la Somali.

Mwandishi: John Juma/ http://APO.af/sdYxnF

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman