Harare:Serikali ya Zimbabwe yaondoa marufuku baadhi ya maeneo
25 Machi 2007Serikali ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, imeondoa kwa sehemu amri ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara iliotangazwa katika maeneo ya mji mkuu Harare. Lakini mkutano wa hadhara uliokua ufanywe leo na chama kikuu cha upinzani Movement for Democratic Change-MDC katika eneo la Mbare mjini Harare umepingwa marufuku. Wakati huo huo shinikizo linazidi kuitaka serikali isitishe hatua za kuwakandamiza wapinzani. Jana vyombo vya habari vya Afrika kusini viliripoti kwamba makamu wa rais wa Zimbabwe Joyce Mujuru alikutana na mwenzake wa Afrika kusini Phumzile Mlambo-Ngcuka mjini Johannesburg, lakini maafisa wakasema mkutano wao ulikua wa kibinafsi. Serikali ya Afrika kusini imekosolewa kwa kile kilichotajwa kuwa ni kubakia kimya kuhusiana na hali ya kisiasa nchini Zimbabwe.