1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE:SADC kutoa ripoti ya hali ya Zimbabwe

1 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBw3

Jumuiya ya Maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika SADC inatarajiwa kutoa ripoti yake kuhusu hali ya kiuchumi na kisiasa nchini Zimbabwe mwisho wa mwezi huu.Kwa mujibu wa katibu Mkuu Tomaz Augusto Salamao mapendekezo ya utafiti wa hali ya Zimbabwe yatatolewa wakati huo.

Bwana Salamao anaongoza kundi la wataalam kutoka jumuiya ya SADC linalotafuta suluhu kwa matatizo ya Zimbabwe inayokabiliwa na mfumko wa bei uliofikia asilimia alfu 3 kwa sasa.

Katika kikao cha mwezi Machi mwaka huu jumuiya ya SADC iliamua kutafuta mbinu za kusaidia taifa hilo ili kurejea katika uchumi wa sawasawa.

Viongozi waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika mjini Dar es Salaam Tanzania walitoa wito kwa mataifa ya magharibi kuiondolewa Zimbabwe vikwazo vya biashara ilivyowekewa serikali.Jumuiya ya SADC aidha ilimpa Rais wa Afrika Kusini jukumu la kuwa msuluhishi katika mvutano kati ya wanasiasa wa upinzani na serikali huku uchaguzi ukipangwa kufanyika mwaka ujao.

Kikao chengine cha SADC kitafanyika nchini Zambia mwezi Agosti na suala la Zimbabwe linatarajiwa kuzungumziwa.