1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE: Zimbabwe yatishia kuwafukuza mabalozi wa mataifa ya magharibi

20 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCHA

Zimbabwe imetishia kuwafukuza mabalozi wa mataifa kigeni. Jana balozi wa Marekani nchini humo, Christopher Dell, alitoka nje ya mkutano aliokuwa nao na waziri wa mashauri ya kigeni wa Zimbabwe.

Christopher Dell aliitwa pamoja na wajumbe wa matifa ya magharibi kuhudhuria mkutano wa waziri wa mambo ya kigeni wa Zimbabwe, Simbarashe Mumbengegwi, ambaye aliwaambia wanadiplomasia hao wanyamae kimya kuhusu kampeni ya serikali ya kuwachakaza wapinzani la sivyo watimuliwe kutoka nchini humo.

Marekani na mataifa ya magharibi yamelaani mashambulio ya hivi karibuni dhidi ya viongozi wanaopinga serikali ya rais Robert Mugabe ambayo imekuwa madarakani kwa miaka 27.

Juzi Jumapili mwanachama wa chama cha Movement for Democratic Change, MDC, alitandikwa alipojaribu kusafiri nje ya Zimbabwe.

Serikali ya rais Mugabe inakabiliwa na shinikizo kubwa huku mfumko wa bei ukifikia asilimia 1,730 na watu wanne kati ya watano wakiwa hawana ajira.