HARARE : Zimbabwe yataka kuungwa mkono na Afrika
23 Machi 2007Zimbabwe iko mbioni kutaka kuungwa mkono na Afrika kunakoyumba yumba wakati shinikizo la kimataifa likizidi kupamba moto dhidi ya Rais Robert Mugabe kutokana na hatua kali za serikali yake kupambana na viongozi wa upinzani.
Katika jaribio la kutaka kuungwa mkono na viongozi wa Afrika Waziri wa Habari wa Zimbabwe Sikhanyiso Ndlovu hapo jana amewaonya dhidi ya kugawanywa na ubeberu ambapo amesema mataifa ya magharibi yamekuwa yakiupakazia uzimwi Zimbabwe kwa kutowa habari za upendeleo za mtizamo mmoja.
Amekishutumu hususan kituo cha televisheni cha Marekani cha CNN kwa kutowa habari za uongo dhidi ya uongozi na serikali ili kuipotosha jumuiya ya kimataifa na kujenga uhasama dhidi ya Zimbabwe.
Wakati huo huo serikali ya Zimbabwe imepinga taarifa kwamba serikali ya Angola itapeleka nchini humo askari wa polisi 2,500 kuimarisha vikosi vya usalama vya nchi hiyo na ubalozi wa Angola mjini Harare pia umekanusha taarifa hiyo.
Serikali ya Zimbabwe imekuwa ikiwaandama kwa kutumia nguvu viongozi wa upinzani wa chama cha MDC ambapo katika siku za hivi karibuni watu kadhaa wamekuwa wakitiwa mbaroni na kupata kisago kikali cha polisi.