HARARE: Washukiwa 8 wazuiliwa na polisi Zimbabwe
9 Julai 2006Watu 8 wamekamatwa na polisi nchini Zimbabwe, wakishukiwa kuhusika na shambulio lililofanywa dhidi ya mwanasheria wa kizungu wa upande wa upinzani nchini humo.Msemaji wa polisi,Wayne Bvudzijena amenukuliwa na gazeti la Sunday Mail akisema kuwa washukiwa 3 walikamatwa kitongoji cha Greendale,ukingoni mwa mji mkuu Harare na wengine walikamatwa Mabvuku mapema wiki hii. Wanamgambo vijana walimshambulia Trudy Stevenson Jumapili iliyopita katika mji wa Mabvuku,kusini mwa Harare.Bibi Stevenson ambae ni mbunge wa upinzani,anaewakilisha eneo la Harare North amesema kuwa alishambuliwa na kundi la wanamgambo vijana wa tawi hasimu la MDC,ambalo ni tiifu kwa kiongozi wa upinzani mkuu,Morgan Tsvangirai.Kambi ya Tsvangirai imejitenga na shambulio hilo na kusema kuwa hakuna ushahidi wa kuwahusisha na tukio hilo.