HARARE. Upinzani nchini Zimbabwe wataka uchaguzi mpya ufanyike.
5 Aprili 2005Matangazo
Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kinataka uchaguzi mpya wa bunge ufanyike nchini humo kufuatia kushindwa kwake kwa mara ya tatu katika uchaguzi wa wiki iliyopita. Chama cha Movement for Democratic Change, kikiongozwa na Morgan Tsvangirai, kilijipatia viti 41 kati ya 120 vilivyoshindaniwa. Msemaji wa chama hicho amesema uchaguzi huo ulikuwa bandia kwa sababu taasisi zote za uchaguzi zilidhibitiwa na chama tawala cha ZANUPF. Mabadiliko ya katiba yalihitajika kukikomesha chama cha rais Robert Mugabe kuzidhibiti taasisi za uchaguzi nchini humo. Chama cha ZANUPF kimeyapinga matakwa ya chama cha MDC, kikiyataja kuwa upuuzi mtupu.