1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE : Mugabe kuwania uchaguzi wa rais ukifanyika 2008

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKB

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe aliyeitawala nchi hiyo kwa muda mrefu amesema katika mahojiano leo hii kwamba anakusudia kugombania uchaguzi wa rais nchini humo iwapo utafanyika kama ilivyopangwa hapo mwaka 2008.

Gazeti la Southern Times linalochapishwa kwa pamoja na kampuni ya magazeti ya New Era ya Windhoek Namibia na ile ya Zimbabwe Newspapers mjini Harare limemkariri Mugabe akisema iwapo chama chake kitasema hivyo atasimama katika uchaguzi huo.

Mugabe mwenye umri wa miaka 83 awali alidokeza kwamba atan’gatuka wakati muda wake utakapomalizika hapo mwakani ikiwa ni miaka 28 baada ya kuchukuwa madaraka kufuatia uhuru wa Zimbabwe kutoka kwa Uingereza hapo mwaka 1980.

Wawakilishi wa serikali za mitaa kutoka chama tawala cha Mugabe cha ZANU-PF walipitisha maazimio hapo mwezi wa Desemba mwaka jana kuongeza muda wa utawala wake kwa miaka miwili zaidi kuwezesha kufanyika kwa pamoja uchaguzi wa bunge na ule wa urais lakini hatua hiyo inabidi iidhinishwe na kamati kuu ya chama pamoja na bunge.

Wakati huo huo polisi wa kutuliza ghasia leo hii wamezuwiya kufanyika kwa mkutano wa hadhara wa kuiombea Zimbabwe na kuwatia mbaroni viongozi wa upinzani akiwemo Morgan Tsvangirai.