Harare. Mugabe kuongezewa muda wa utawala.
15 Desemba 2006Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, anasemekana kuwa anaunga mkono mipango ya chama chake ya kurefusha muda wa urais wake kwa zaidi ya miaka miwili hadi mwaka 2010. Pendekezo hilo linaweza kuungwa mkono katika mkutano wa mwaka wa chama tawala cha ZANU-PF mwishoni mwa wiki hii.
Mugabe mwenye umri wa miaka 82, amekuwa akisema mara kwa mara kuwa atang’atuka ifikapo mwaka 2008, hata hivyo chama chake kinataka kubadili utaratibu wa uchaguzi ili uchaguzi wa bunge na rais ufanyike wakati mmoja mwaka 2010. Msemaji wa chama cha ZANU-PF amesema kuwa hatua hiyo itaokoa fedha. Mugabe ameitawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 28, kukiwa na ukosefu mkubwa wa kazi na ughali wa maisha unaofikia kiasi cha asilimia 1,000 kiwango kikubwa kabisa duniani.