1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE: Mugabe atoa matamshi makali dhidi ya wakosoaji wake

16 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIU

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amewaambia wakosoaji wake waende kujitia kitanzi. Mugabe ameushambulia kwa maneno ukosoaji uliotolewa ulimwenguni kote dhidi yake baada ya kukamatwa na kuteswa kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai.

Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 83 amekilaumu chama kinachoongozwa na Tsvangirai cha Movement for Democtratic Change, MDC, kwa kuchochea machafuko yaliyosababisha kukamatwa kwake Jumapili iliyopita.

Morgan Tsvangirai amekuwa akiendelea kupata matibabu hospitalini tangu Jumatatu wiki hii kwa majeraha mabaya aliyoyapata alipokuwa akizuiliwa na polisi. Mke wa Tsvangirai, amesema kwa sasa mumewe hajambo.

´Yuko katika hali nzuri. Hali yake imeimarika na sasa yuko salama anajisikia nafuu. Madkatari wanasema mume wangu yuko katika hali nzuri zaidi kuliko hapo awali. Hayuko tena katika hatari kwa sasa.´

Katika taarifa iliyochapishwa leo na gazeti la Independent, mjini London Uingereza, Morgan Tsvangirai ameapa kuendelea kupigania uhuru kutoka kwa rais Robert Mugabe licha ya kupigwa na polisi.