1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE : Mugabe aonya kufyetulia risasi wapinzani

15 Agosti 2006
https://p.dw.com/p/CDLM

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameonya wapinzani leo hii kwamba jeshi la Zimbabwe liko tayari kufyetuwa risasi dhidi ya yoyote yule anayetaka kumpinduwa wakati mgogoro unaozidi kupamba moto wa kisiasa na kiuchumi ukizidisha hofu ya kuzuka kwa machafuko nchini humo.

Viongozi wa upinzani mwaka huu wametowa wito wa kufanyika kwa maandamano ya mitaani kukomesha utawala wa muda mrefu wa Mugabe ambao wanasema umeigeuza nchi hiyo ambayo hapo zamani iliwahi kuonekana kuwa mojawapo yenye mategemeo makubwa barani Afrika kuwa ile yenye kuomba chakula.

Lakini maandamano hayo bado kuanza na kuwafanya wachunguzi wa kisiasa wajiulize iwapo Wazimbabwe wana hofu mno tu kufikisha manun’guniko yao barabarani.

Mugabe akizungumza katika maandamano ya kuadhimisha Siku ya Majeshi amedokeza kwamba hofu hizo yumkini zinaweza kuwa za kweli.

Amesema anataka kuwakumbusha wale ambao yumkini wanaficha mipango yoyote ile ya kuigeukia serikali watambuwe kwamba kuna wanajeshi waume kwa wake wanaoweza kufyetuwa risasi.