HARARE-Mamluki waliokuwa kifungoni Zimbabwe waachiwa huru.
11 Mei 2005Serikali ya Zimbabwe leo imewaachia huru wageni 62,ikiwa ni zaidi ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya wageni hao kukamatwa kwa tuhuma za kupanga njama za kuiangusha serikali ya Guinea ya Ikweta.
Kikundi hicho cha wafungwa wa kigeni kilichokuwa kikisafiri kwa kutumia hati za kusafiria za Afrika Kusini,kilikamatwa mjini Harare mwezi Machi mwaka jana,baada ya ndege yao kuzuiwa iliposimama kwa muda katika uwanja wa ndege wa Harare.
Baadae watu hao walishtakiwa kwa kukiuka sheria za uhamiaji na makosa mengine ya kukutwa na silaha na adhabu zao zinamalizika leo.
Serikali ya Guinea ya Ikweta iliwahukumu raia wa kigeni 11 mwezi wa Novemba mwaka jana,vifungo vya kati ya miaka 14 na 34 kwa makosa ya kula njama za kufanya mapinduzi,watu hao wakiwa wamehusishwa na waliokamatwa Zimbabwe.
Nchini Afrika Kuasini,Mark Thatcher mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza,Margareth Thatcher alilazimika kukiri mwezi wa Januari,kula njama za kusaidia mpango huo wa mapinduzi,chini ya makubaliano ya kumuepusha na kifungo,chini ya sheria ya kupambana na askari mamluki ya Afrika Kusini.