Harakati za majeshi ya Pakistan dhidi ya vikosi vya taliban
19 Oktoba 2009Hali nchini Pakistani bado ni tete, mapigano yameendelea kushamiri baina ya majeshi ya serikali na yale ya waasi wa kikundi cha Taliban, ambapo hii leo jeshi la nchi hiyo likisaidiwa na vikosi vya mizinga limewashambuliwa waasi hao na kulishikilia eneo walilokuwa wakilidhibiti kwenye mpaka na Afghanistan.
Mapigano hayo ni jaribio jipya la mpango wa serikali wa kujaribu kukabiliana na mfululizo wa mashambulizi ya waasi yanayoelekezwa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo, likiwemo lile lililofanywa katika makao makuu ya jeshi la nchi hiyo, ambalo liliua takribani watu 150.
Mzozo huo unaoangaliwa kama kitovu cha dunia cha wapiganaji wa kiislamu, unafuatiliwa kwa karibu na Marekani pamoja na mataifa mengine yenye nguvu duniani, na tayari kamanda wa majeshi ya Marekani katika ukanda huo David Petraeus, yuko nchini Pakistan kwa mazungumzo hii leo.
Vikosi vya serikali vimedai kupata maendeleo makubwa katika mapigano ya leo katika eneo la Kusini la Waziristan, na wachambuzi wa masuala ya kivita wanatarajia vikosi vya serikali kupata upinzani hafifu, kwa sababu majeshi ya wataliban yamesogezwa kutoka katika eneo walilokuwa wanalidhibiti.
Kamanda mkuu wa vikosi vya serikali Athar Abbas, akielezea hali halisi ya mapigano hayo, amesema:
"Ni vigumu kwa kweli kuelezea hali halisi ya upinzani, lakini kuna upinzani, na vikosi vinaendelea vizuri. Katika wakati kama huu ni vigumu kujua idadi kamili ya wapiganaji waliojeruhiwa au kuuawa. Kuna upinzani, na vikosi vya ulinzi vinasonga mbele."
Amesema waasi wanaweza pengine kutumia mabomu mazito zaidi katika maeneo yanayolengwa na vikosi vya serikali, lakini kama wakitolewa katika eneo wanalolidhibiti, ambalo ndio nguzo yao ya kuanzishia mashambulizi, kuna uwezekano wakakimbia kabisa.
Hii leo wakaazi wa Wana, ambalo ni eneo mashuhuri zaidi Kusini mwa Waziristan, wamesema kulikuwa na mapigano makili zaidi kuwahi kushuhudiwa usiku wa kuamkia leo.
Jeshi la nchi hiyo lilisema jana kuwa wapiganaji 60 na wanajeshi watano wa vikosi vya serikali, waliuawa katika saa 24 za mwanzo za mapigano hayo.
Taarifa zinasema vyombo vya habari vya kigeni haviruhusiwi kuingia katika eneo hilo, na ni hatari hata kwa vyombo vya habari vya nchi hiyo pia.
Jeshi la nchi hiyo lilianzisha shambulizi la mara ya kwanza dhidi ya Taliban Kusini mwa Waziristan mwaka 2004, ambapo lilishuhudia wanajeshi wake wakishambuliwa vikali, kabla ya kupendekeza makubaliano ya amani.
Lakini wachambuzi wanasema wakati huu, jeshi hilo, serikali na umma kwa ujumla, wote wanaafiki kuwa wakati sasa umefika wa kulishughulikia kundi la Taliban lililoko Pakistan.
Marekani imekuwa ikiishinikiza serikali ya Islamabad kuwatawanya wapiganaji wa Taliban na al Qaeda katika ukanda huo, ambao hutumiwa na wapiganaji hao kupanga mipango ya mashambulizi dhidi ya vikosi vya kigeni nchini Afghanistan.
Kamanda David Petraeus wa vikosi vya Marekani, amethibitisha kuwa majeshi ya Pakistan yamepata maendeleo makubwa katika mapigano ya leo.
Mwandishi:Lazaro Matalange/DPA/RTRE
Mhariri:Abdul-Rahman.